Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Desemba, ni fursa muhimu ya kuhamasisha jamii na dunia kwa ujumla kuhusu haki, usawa, na ustawi wa watu wenye ulemavu
Katika kuadhimisha siku hiyo, Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kimeandaa semina na kimetoa elimu kwa wanafunzi kuhusu haki za watu wenye ulemavu na namna wanavyoweza kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo kwenye sekta ya elimu, huduma za afya, ajira na ushirikishwaji kwenye masuala ya kijamii
Katika Semina hiyo, Naibu Mkuu wa Chuo taaluma, tafiti na ushauri wa Kitaalam, Prof. Epaphra Manamba amesmea kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kinajitahidi kila mwaka kuwatambua na kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu kwa kuboresha miundombinu, kuanzisha sera maalum, kuboresha mitaala itakayotoa elimu jumuishi na kutoa huduma za kitaalam kama kuongezewa muda wakati wa mitihani na kuwajumuisha wakalimani wa lugha ya alama na huduma nyingine muhimu, ili kuwasadia wakati wa masomo.
Aidha, Prof. Manamba amesisitiza kwamba binadamu wote ni sawa na kuwaasa wanafunzi wasiwabague na kuwanyapaa watu wenye ulemavu, kwani wana mchango mkubwa katika maendeleo ya chuo, jamii, na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa idara ya elimu na mratibu wa elimu jumuishi Godwin Urio, amesema kuwa IAA ina zaidi ya wanafunzi 50 wenye ulemavu, ambapo Chuo kimeandaa miongozo ya kusimamia wanafunzi hao na lakini pia wameanzisha ofisi yenye wataalamu wa elimu maalum na saikolojia kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu.
Dkt. Lwimiko Sanga, mtaalamu wa saikolojia jamii na elimu maalum kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), amehimiza jamii kuachana na imani potofu kuhusu ulemavu na kuwasaidia watu wenye ulemavu, na kuwa ni wajibu wa kila mtu kuwapenda na kuwasaidia waweze kufikia ndoto zao.
Nao baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wameshukuru semina hiyo kwa kuwajengea kujiamini na kutambua uwezo wao katika jamii, huku wakisifu juhudi za chuo katika kuweka mazingira rafiki ya kujisomea na kufanikisha malengo yao.