Na John Walter -Babati
Wakati tunaumalizia mwaka 2024, tasnia ya soka mkoa wa Manyara imezua gumzo kubwa baada ya waliokuwa wagombea kuondolewa kwenye nafasi hizo huku mmoja akitajwa sio mtanzania halali.
Mgombea huyo ambaye ni mpaka sasa ni mwenyekiti wa Chama cha mpira wa miguu wilaya ya Babati kwa miaka nane Gerald Romli Mtui, ameenguliwa kwenye mchakato kwa kutumia kanuni ya uchaguzi ya TFF (ELECTRICAL CODE) Toleo la 2021 Kanuni ya 9 kipengele kidogo cha 1 kinachoeleza kuwa mgombea Sharti awe Mtanzania.
Licha ya Gerald kwenye fomu yake ya maombi kuambatisha nakala ya cheti cha kuzaliwa na nakala ya kitambulisho cha NIDA lakini bado Kamati haijataka kuelewa.
Aidha Kamati imemwondoa mgombea huyo kwa maelezo kuwa hakidhi kanuni ya 9 kipengele kidogo cha 7 kinachoelezea maswala ya kukosa uadilifu.
Mgombea mwingine ambaye ameenguliwa ni Yusufu Mdowe ambaye ni Kiongozi wa Chama cha Soka mkoa wa Manyara anayemaliza muda wake na amekuwa kiongozi kwa kuchaguliwa kwa kupigiwa kura kwa zaidi ya miaka 14.
Mdowe ameenguliwa kwa kanuni ya 9 kipengele kidogo cha 2 kinachosema mgombea walau awe na elimu ya kidato cha nne, asiwe amewahi kukutwa na Kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo mahakamani na kutumikia kifungo magereza bila hata nafasi ya kulipa faini kwa mujibu wa kipengele kidogo cha 4 kipengele kidogo cha 7 kinachozungumzia Uadilifu.
Wagombea wengine wameenguliwa kwa kanuni hiyo hiyo ya 9 na vipengele vyake vidogo vya 2,4 na 7 vinavyoeleza maswala ya elimu ya kidato cha nne,kuhukumiwa mahakamani na kukosa uadilifu wakati wagombea hao wamewahi kuwa Viongozi na hata sasa ni viongozi kwenye mchezo wa soka kwa ngazi tofauti na baadhi yao ni watumishi wa umma na sio tu watumishi wa umma bali ni viongozi wakubwa ndani ya ofisi za serikali.
WASIWASI NA MASHAKA YA WAZALENDO WA SOKA MANYARA.
Kamati imetumia kanuni za uchaguzi za TFF (ELECTRICAL CODE) Toleo la 2021 Kinyume na utaratibu kwani vifungu walivyonukuu kwa kila mgombea aliyeenguliwa havina ukweli wala hawana Ushahidi wowote wa mapungufu hayo ya wagombea.
Inahisiwa kanuni hii kutumika kwa lengo la wakuwatisha na kuwaogombesha wagombea kwa kuwa wanatajiwa kuwa ni kanuni za TFF,Na ukitaka kukata rufaa Sharti ulipe MAMILIONI YA PESA,pia kamati ikidhani wagombea hawana uwezo wa kuziona na kuzirejea kanuni husika.
Kamati ya uchaguzi ya MARFA imekiuka taratibu za uchaguzi kwani wao wanahusika na kuendesha uchaguzi pekee na sio kushughulika na maswala ya MAADILI YA WAGOMBEA,MARFA inapaswa kuwa na kamati ndogo ya Maadili ili kama kungebainika maswala yeyote ya kimaadili basi yangefanyiwa kazi na kuamuliwa na kamati ya maadili na wao kupewa majibu na kufanyia kazi hatua zilizochukuliwa na kamati ya maadili
Kama kweli wagombea hawa wangekuwa wanakosa sifa hizo tena ambazo nyingine ni nzito kwa mujibu wa sheria basi wagombea walikuwa na haki ya kuitwa mbele ya kamati husika na kupata haki ya kujisafisha na kujitetea kabla ya kamati kufanya maamuzi.
Inaonekana wazi kuwa wagombea waliopitishwa na kamati ya uchaguzi ni wale waliokuwa madarakani na wanamaliza muda wao sasa,Kitendo hiki kinaonesha wazi kuwa huu ni mkakati wa makusudi wa kuwarudisha waliokuwa madarakani kwani aliyepitishwa kwa nafasi ya mwenyekiti alikuwa mjumbe wa MARFA Kwenda TFF, aliyepitishwa kuwa mjumbe wa MARFA Kwenda TFF hata sasa ni mjumbe wa kuteuliwa wa Mkutano mkuu TFF,waliopitishwa kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF Mmoja alikuwa Makamu wa mwenyekiti na mwingine alikuwa mweka hazina wa chama.
Mantiki ya kawaida inatuongoza kuwa huu ni mpangilio maalum uliondaliwa na kutekelezwa na kamati ya uchaguzi kuwa walio ndani ya MARFA waendelee kubakia ndani ya MARFA na walio nje KAMWE hawapaswi hata kuchungulia na kuona huko ndani ya chama kunafananaje.
Kamati hii hii ya uchaguzi kwenye uchaguzi wa MARFA uliopita wa Septemba, 2020 ndiyo iliyosimama kidete kuvuruga na kuharibu uchaguzi uliofanyikia wilaya ya Hanang na kulazimisha kuingiza madarakani viongozi hawa leo wanaofanya tena hujuma ya kurudi madarakani kwa mbinu ya kidhalimu ya kuinunua kamati ya uchaguzi, Viongozi hawa wanaodai kuwapitisha leo TAYARI WALISHAFELI PAKUBWA SANA KWENYE UONGOZI KWANI,Toka mwaka 2020 hakuna Mpira wowote ule wa miguu unaochezwa ndani ya mkoa wa Manyara,Hakuna Ligi za kisheria zinazochezwa sio ligi Daraja la nne wala la tatu, hakuna mpango mkakati wowote wa maendeleo ya soka unaoandaliwa na kutekelezwa ndani ya wilaya na Mkoa, hakuna vikao vyovyote vya kisheria vinavyokaliwa na kujadili maendeleo ya soka, hakuna taarifa zozote za mapato na matumizi vinazofahamika, KWA UJUMLA VIONGOZI HAWA WALISHAUUA MPIRA WA SOKA WA MANYARA Wanachotafuta sasa ni nafasi ya kuja kuufanyia MAZISHI ili nafsi zao zifurahi na kusherehekea.
USHAURI WA WAZALENDO WA MANYARA NA WAPENDA MAENDELEO YA SOKA KUHUSU SAKATA HILI.
Tunazishauri mamlaka husika za mchezo wa soka na Serikali ngazi ya Mkoa na Taifa kwa haraka kuliona hili na kuingilia kati mchakato huu ili uchaguzi usimamishwe ili kujipanga upya na uchaguzi usimamiwe na chombo huru kwa lengo la sheria taratibu na kanuni za uchaguzi kwenye mchezo wa soka kuzingatiwa ili wachaguliwe viongozi wanaokubalika na wenye uwezo wa kuleta maendeleo ya soka ndani na nje ya Mkoa wetu.