Na.Alex Sonna-DODOMA
WATAALAMU wa MipangoMiji wamejifungia kwa siku mbili jijini Dodoma kuweka mikakati namna ya kuhakikisha mipango iliyowekwa inadumu.
Akizungumza leo Disemba 3,2024 jijini Dodoma kwenye mkutano mkuu wa tisa wa Mwaka wa Maofisa Mipangomiji Tanzania, Naye, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji, Lucas Mwaisaka, alisema katika mkutano huo wataalam hao wanajifanyia tathmini na kupata elimu namna ya kusimamia mipango wanayoipanga ili kuondokana na tatizo hilo.
“Tumejadili namna ya kutumia teknolojia kusimamia shughuli zote za Mipangomiji, tumefanya kazi kubwa ya kuanzisha mfumo ambao umeunganishwa na e-ardhi ili kudhibiti na kufanya kazi kwa haraka kuwahudumia wananchi kupitia mifumo,”alisema.
Alisema tangu bodi hiyo ianze kufanya kazi Mwaka 2009 imesajili kampuni 101 na wataalamu 546 huku kampuni 11 na wataalamu 32 wamefutiwa usajili kutokana na kukiuka sheria ya mipango miji kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC),Bw. Joseph Mafuru, alisema upimaji na upangaji shirikishi wa moja kwa moja kwa wananchi kwenye mitaa na vijiji nchini ndio mwarobaini wa kuondokana na wimbi la ubadilishaji wa matumizi ya ardhi iliyopangwa.
Alisema kuna umuhimu kusimamia mipangomiji kuanzia kwa wananchi kwenye mitaa husika ili kuimarisha na kulinda maeneo hayo yasibadilishwe matumizi.
“Tumejifungia hapa wataalamu kuangalia njia gani tutumie kwenye ‘development control’ hili ni muhimu kwasasa kama mtakumbuka kuna wakati Jiji la Dar es salaam waliweka utaratibu wa kubandika kwenye mitaa ramani ya mipangomiji ambayo ilikuwa inaonesha maeneo ya makazi, biashara, viwanja vya michezo, maeneo ya kupumzikia, shule, hospitali na huduma zingine za msingi, hii inasaidia kuwafanya wananchi wa eneo husika kulinda maeneo hayo muhimu kwenye mitaa yao,”alisema.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wataalam wa Mipangomiji (TITA), Emanuel Luhamba, aliomba serikali kutoa kipaumbele kwenye sekta ya ardhi hususan kwenye mipangomiji kwa kuwa ni uumbaji mwingine wa pili baada ya Mungu.
“Kuna changamoto kubwa zinaikumba sekta ya mipangomiji ikiwamo uhaba wa rasilimali fedha ambazo zingewezesha kupima na kupanga miji yetu na vijiji kwa kuwa vijiji vya leo ndio miji ya kesho, fedha hizi wakati mwingine zinahitajika katika kutwaa maeneo ili yawe wazi uweke mipangomiji inayofaa,”alisema.