Na WAF, IRINGA
Mkurugenzi Idara ya Tiba wa Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea amesema wananchi zaidi ya 800 wamehudumiwa ndani ya saa 24 katika kambi ya Madaktari Bingwa kwenye Hospitali ya Rufaa Iringa.
Dkt. Nyembea ameyasema hayo Desemba 3, 2024 wakati alipofanya ziara ya kujionea hali ya utoaji wa huduma na kuridhishwa na mwenendo wa kambi ya Madakatari Bingwa kwenye Hospitali ya Rufaa Iringa iliyowekwa kwa Kanda ya Kati na zinazoendelea kwenye kanda tano kwa sasa nchini.
Dkt. Nyembea amesema mpango huo wa kambi za Madaktari Bingwa umeonesha mafanikio makubwa kwa kusogeza huduma muhimu za kitabibu karibu na wananchi.
“Shabaha ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wa chini walioshindwa kugharamia huduma za kibingwa wanapata fursa hiyo, hapa tumeshuhudia wananachi wakisubiri kupatiwa huduma huku wengi wao wakiishukuru Serikali kwa kuja na wazo hili la kambi ya madaktari bingwa kwenye hospitali mbalimbali nchini, hii ni ishara kwamba huduma hizi wanaziitaji,” amesema Dkt. Nyembea.
Dkt. Nyembea ameongeza kuwa zaidi ya watu 5000 wamehudumiwa kwa siku moja kwa kanda zote tano za Ziwa mkoani Mara, Rukwa kanda ya Magharibi, Kilimanjaro Kanda ya Kaskazini, Njombe kwa Nyanda za Juu Kusini na Hospitali ya Rufaa Iringa iliyowekwa kwa Kanda ya Kati .
Timu ya madaktari bingwa na wabobezi 56 wamepiga kambi katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani.