Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Viongozi wa dini mkoani Arusha wameipongeza Tume huru ya Taifa ya uchaguzi kwa kuwakutanisha wadau wa uchaguzi na kuwaelimisha juu ya Uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura .
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Sheikh Haruna Hussein, ambaye ni Msemaji wa Taasisi ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriya Razikia Jailania Tanzania, ametoa wito kwa wananchi na viongozi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwani jambo hilo ni jema sana kwa kuwa kiongozi akielewa basi ni rahisi kuelimisha watu anaowaongoza ndani ya maeneo yao.
“Tunafahamu kuwa kwa mujibu wa ibara ya 74(6) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,Tume imepewa mamlaka ya kutekeleza majukum mbali mbali,ikiwa ni pamoja na jukumu la kusimamia na kuratibu Uandikishaji wa Wapiga kura kwaajili ya Uchaguzi wa Raisi na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania bara.”amesema .
Jukumu hilo pia limewekwa kwenye kifungu cha 16 (5) cha sheria ya Uchaguzi wa Raisi , Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024,ambacho kinaweka sharti kwa Tume Kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya Uchaguzi mkuu uliomalizika na kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea kwaajili ya Uchaguzi mkuu unaofuata.
Hivyo basi kwa kuwa ni takwa la kisheria tunaomba wananchi tujitokeze kuweka taarifa zetu sawa kwa wale waliohama kutoka eneo moja hadi jengine, wapo wengine watatimiza miaka 18,mwakani 2025 hao nao ni wadau muhimu sana wasibakie nyuma kuweka Taarifa zao .
“Sisi kama wadau tunaiomba Tume iendelee kutoa elimu katika maeneo mengine kwa kadiri inavyowezekana na nimesikia kauli mbiu ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga kura kwa mwaka 2024/25 ni “Kujiandikisha kuwa Mpiga kura ni Msingi wa Uchaguzi bora” ndugu zangu watanzania na wakazi wa
mkoa wa Arusha,Kilimanjaro na Dodoma.”amesema .
“Kwa umoja wetu Twendeni tukahakiki taarifa zetu usiache ni muhimu sana kwa msingi wa maendeleo ya nchi yetu na Tunawaomba sana Vyama vyote tuendelee kuelimisha wafuasi wetu, Viongozi wa dini na viongozi wa Mila tusiache kuhamasisha jamii.”amesema .
Aidha Sheikh Haruna ametoa wito kwa Tume kuhakikisha kuwa inafika mpaka vijijini ili kila mtanzania anayehitajika kufikiwa na Zoezi hili wapatiwe elimu ya kutosha .
Ameongeza kuwa ,ni vizuri wakatoa kipaumbele kwa makundi maalumu wajawazito,wanawake wenye watoto wachanga na ndugu zetu walemavu washirikishwe katika kuhakikisha kuwa wanatengenezewa mazingira mazuri kwa ajili ya zoezi hili .
Kwa upande wake Mchungaji Yohane Parkipumi wa Kanisa la Moraviani amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha amani na kutoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za kulinda na kuimarisha amani na ninawaomba wachungaji, mashehe na viongozi wa mila kuendelea kuliombea taifa hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao,” amesema Mchungaji Parkipumi.
Naye Sheikh Iddy Ngella amehimiza wananchi kutumia fursa ya amani iliyopo kukuza uchumi wa taifa.
“Mahusiano mazuri kati ya Tanzania na majirani zake yanayojengwa na viongozi wetu ni fursa ya kukuza uchumi. Wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla, tumieni amani hii kuboresha maisha yenu na ya taifa,” alisema Sheikh Ngella.
Viongozi hao wa dini wamewataka wananchi wote kuhakikisha wanahakiki na kuboresha taarifa zao kwa wakati ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.