*📌Wananchi 3,255 kila wilaya ya mkoa huo kunufaika*
Wakala wa Nishati Vijiji (REA) kupitia kampuni ya Manjis Logistics Ltd, imeanza rasmi Mradi wa kusambaza majiko ya gesi 22,785 kama sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha na kuwawezesha Watanzania, kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia katika mkoa wa Kagera.
Msimamizi wa Miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi, Deusdedith Malulu, amemtambulisha rasmi, msambazaji wa majiko hayo kwa mkoa wa Kagera, kampuni ya Manjis Logistics Ltd mbele ya Katibu Tawala wa mkoa huo, Bwana Stephen Ndaki katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, tarehe 30 Novemba, 2024.
Mhandisi Malulu amesema, utekelezaji wa Mradi wa kusambaza majiko ya gesi kwa mkoa wa Kagera unaenda sambamba na malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei mwaka wenye lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 kwa Watanzania, ifikapo mwaka 2034.
“REA imeingia mkataba na Mtoa huduma, kampuni ya Manjis Logistics Limited ambayo itahudumia wilaya zilizopo ndani ya mkoa wa Kagera kwa kuuza kwa bei ya ruzuku, mitungi ya gesi ya kilo sita (6) pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji”. Alisema, Mhandisi, Malulu.
“Kwa mkoa wa Kagera, Serikali kupitia REA inatekeleza Mradi wa kusambaza majiko 22,785 yenye thamani ya shilingi milioni 378 ambapo mtungi wa gesi pamoja na vifaa vyake, ulikuwa uuzwe shilingi 35,000 lakini sasa kwa bei ruzuku, Wananchi watanunua mtungi wa gesi pamoja na jiko lake kwa shilingi 17,500. Sharti kubwa la kupata majiko hayo ni lazima Mwananchi awe na Kitambulisho ya Taifa (NIDA) au namba ya NIDA”. Amesisitiza Mhandisi, Malulu.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera, Bwana Stephen Ndaki ameishukuru REA kwa kufanikisha Mradi huo wa majiko ya gesi pamoja na vifaa vyake na kuongeza kuwa majiko ya gesi, yatasaidia Wananchi wa mkoa wa Kagera kuendelea kuhamasika kutumia nishati safi ya kupikia.
“Ninawaomba REA kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia lakini pia tunaomba muongeze idadi ya majiko ya gesi pamoja na majiko banifu, tunaomba pia spidi iongezeke kwa mkandarasi anayetekelza Mradi wa kufunga miundombinu ya umeme wa jua kwa Wananchi wetu wa kisiwa cha Musila”. Amekaririwa Bwana Ndaki.
Mkoa wa Kagera una jumla ya wilaya 7; wilaya hizo ambazo Wananchi wake watanufaika na majiko hayo gesi ni pamoja na wilaya ya Bukoba, Biharamulo, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Muleba na Ngara.