Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatumia nafasi zao ipasavyo kuhamasisha utalii nchini hususani kwa waumini wao ili kuongeza idadi ya watalii na kufikia azma ya serikali ya watalii milioni tano na mapato ya dola bilioni 6 ifikapo 2025/2026.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Jully Lyimo katika hafla ya uzinduzi wa Tisheti Mpya iliyoandaliwa na Taasisi ya dini ya kiislamu ya Twarika, iliyolenga kuhamasisha utalii wa ndani kupitia kauli mbiu isemayo ‘Viongozi wa dini uhifadhi endelevu’, .
Amesema kuwa ,viongozi wa dini Mkoa wa Arusha wameanza kampeni ya kuhamasisha utalii
na upandaji wa miti ,na kwa kuanzia
wamepanga kupanda miti 10,000 ikiwa ni
mpango wa kuboresha mazingira katika
maeneo ya akiba na mpango huo unapaswa kuigwa na viongozi wote wa dini nchini,
Kamishna Lyimo amesema Viongozi hao wana nafasi kubwa kwenye jamii kupitia mafundisho yao ambayo yameendelea kuwa na tija katika kuendeleza uhifadhi na kuhamasisha utalii wa kutembelea Hifadhi mbalimbali nchini.
Hata hivyo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii popote watakapokuwa ili wananchi waweze kupata uelewa wa kutosha kuhusu vivutio vyetu na hatimaye kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza nchi yetu na kazi zinazofanywa na Rais Samia .
“Viongozi wa dini mmekuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata nyayo za Rais wetu Samia Suluhu Hasan ambaye amekuwa mhifadhi wa kwanza kupitia filamu yake ya The Royal Tour” amesema Lyimo.
Amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwahamasisha waumini wao ili kuweza kutembelea vivutio mbalimbali vya utali hapa nchini huku akisema kuwa Tanapa itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kukuza sekta ya utali hapa nchini,
Kwa upande wake Kiongozi wa Taasisi ya Twarika Sheikh Haruna Husein amesema kuwa wajibu wa viongozi wa dini ni pamoja na kuelezea umuhimu wa sekta ya utali katika kukuza uchumi wa nchi yetu.
Amesema viongozi wa dini wanawajibu mkubwa wa kumuunga mkono Rais Samia ambaye amekuwa Rais wa kwanza kuhamasisha utalii kupitia filamu ya Rayol Tour ambayo aliicheza mahususi kutangaza vivutio vyetu hapa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Viongozi wa Dini Mchungaji Zelote Pallangyo amesema kuwa wanaungana na jitihada za serikali katika kuendeleza nchi kwa maendeleo endelevu na mikakati ya utunzaji wa mazingira kutokana na uumbaji wa Mungu.