Mwanasiasa na Mfanyabiashara Enock Koola, ambaye ni Mdau wa Maendeleo katika Jimbo la Vunjo, Mkoani Kilimanjaro, amepongeza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa usimamizi mzuri wa zoezi la upigaji kura nchini.
Koola, ambaye pia ni Mfanyabiashara Mkubwa na Kiongozi Mwandamizi wa Siasa Kijana, alitoa pongezi hizo leo, Novemba 29, 2024, kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kwa kuongoza kwa ufanisi zoezi hilo la kihistoria. Alieleza kuwa usimamizi mzuri wa TAMISEMI umewezesha wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wanaowahitaji, bila ya kuvurugika kwa amani yoyote.
“Binafsi, naipongeza TAMISEMI kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kusimamia zoezi hili kwa ufanisi. Hii ni ishara kwamba wananchi wanatambua umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na wameonyesha utulivu mkubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Zoezi hili limeendeshwa kwa amani na bila ya taharuki yoyote,” alisema Koola.
Kwa upande mwingine, Koola alitolea mfano wa mafanikio ya uchaguzi katika vyama vyote 19 vya siasa, vilivyoshiriki katika kutoa wagombea wa serikali za mitaa, vitongoji, na vijiji, kwa lengo la kukuza demokrasia na kutoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi kwa amani na utulivu.
“Ushindi wa kishindo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni matokeo ya kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa Ilani ya CCM. Rais Dkt. Samia ameweka mbele miradi ya maendeleo na fursa za ajira kwa vijana, na hii inathibitisha mafanikio ya Serikali ya CCM,” aliongeza Koola.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Koola alifurahishwa na matokeo ya uchaguzi, ambapo CCM ilishinda vijiji vyote 157, vitongoji 689, huku vyama vya upinzani vikipata vitongoji 9 pekee. Pia, aligusia kitongoji kimoja cha Kata ya Kibosho Magharibi ambapo uchaguzi uliahirishwa baada ya mgombea mmoja kufariki.
“Hii ni ishara wazi kuwa wananchi wa Wilaya ya Moshi, Jimbo la Vunjo, wameonyesha dhamira ya dhati katika kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu,” alisema Koola.
Aliongeza kuwa, serikali inapaswa kuendelea kushirikiana na wananchi na vyama vya siasa katika kuhakikisha kuwa uchaguzi uendelee kufanyika kwa amani na utulivu, na kutoa shukrani kwa jeshi la polisi kwa kuzingatia usalama wakati wa mchakato wa upigaji kura.
“Hii ni fursa ya pekee kwa wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kujenga taifa letu. Tumekuwa na mafanikio makubwa, lakini tunahitaji kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana kama Watanzania,” alisisitiza Koola.
Aidha Koola alitoa wito kwa watu kuendelea kushiriki chaguzi zijazo ambazo zitaleta taswira mpya ya Taifa letu na kukuza Demokrasia ya Nchi Yetu Kwa kutumia Uhuru wa kuchagua kiongozi Ambaye unamuhutaji
Aliwaomba Wananchi Kuwa Mchakato wowote ambao unaendeshwa hapa Nchin tukubali kuwa mapungufu hayakosekani maana watekelezaji ni binadamu, Lakini natoa wito kwa pande zote kuendelea kuwekeza kwenye maandalizi mazuri kwa muda mrefu ili kuendelea kupunguza changamoto ambazo zinajitokeza kwenye chaguzi zetu.alisema koola