Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Juma Mkabakuli, akifungua Kongamano la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa niaba ya Uongozi wa Wizara ya Fedha lililofanyika Mkoa wa Mbeya.
Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Juma Mkabakuli, akitoa ufafanuzi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara mbalimbali (hawamo pichani) wakati wa Kongamano la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoa wa Mbeya. Kushoto kwake ni Afisa Mwandamizi wa Kodi kutoka Idara ya Utafiti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Bw. Robert Manyama pamoja na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Mkoa wa Mbeya Bw. Musibu Shabani.
Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Juma Mkabakuli (kulia) akiandika maoni yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo – TCCIA Mkoa wa Mbeya Bw. Erick Sichinga (kushoto).
Mjasiriamali wa Viwanda Vidogo vya Kusindika Unga wa Mayai, Bi. Elizabeth Kalinga akitoa maoni kuhusiana na maboresho ya kodi kwenye viwanda vidogo vidogo, kwenye Kongamano la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoa wa Mbeya.
Mhasibu Daraja la Kwanza Bw. Nghabi Mbogo, kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoulizwa kuhusiana na Ushuru wa Huduma (Service Levy), wakati wa Kongamano la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoa wa Mbeya.
Mjasiriamali Mdogo wa Vyakula vya Lishe Bi. Sophia Mrwati akitoa mchango wake kuhusiana na Ubora wa Bidhaa wakati wa Kongamano la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoa wa Mbeya.
Wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo, sekta ya kilimo, biashara za usindikaji wa mazao na washauri wa kodi wakisikiliza wasilisho (halionekani pichani) lililotolewa na Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha Bw. Mathias Kadebe,(Aliyesimama) kuhusiana na maoni yaliyofanyiwa kazi katika Makongamano ya Kodi Kikanda yaliyofanyika mwaka jana (2023), katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mbeya)
……
Na. Eva Ngowi, WF – Mbeya
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wa sekta binafsi katika uwekezaji, na imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini.
Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Juma Mkabakuli, wakati wa Kongamano la Kodi lililofanyika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoa wa Mbeya.
Bw. Mkabakuli alisema, ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi, Serikali inaendelea kuboresha Mazingira ya biashara nchini na imefuta na kupunguza baadhi ya ada na tozo kero takriban 379.
Alisema, Serikali inaendelea kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla; kuwa na sera za kodi zinazotabirika na kuwianisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza na kurahisisha ulipaji wake kupitia namba ya malipo jumuishi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo- TCCIA Mkoa wa Mbeya, Bw. Erick Sichinga, alisema wanaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kuwa na majukwaa hayo kila mwaka kujadili sera za kodi.
“Mbeya tumebahatika kuwa moja kati ya mikoa ambayo Makongamano haya yanafanyika, nikilinganisha na Kongamano ambalo lilifanyika mwaka jana na mwaka huu nimeona kuwa kuna maendeleo makubwa ambayo sisi wadau wa sekta binafsi, tumeona Serikali imeanza kuwa sikivu, kero mbalimbali zimeanza kufanyiwa kazi, tumeona baadhi ya Maafisa wakipita katika sekta binafsi kwa ajili ya kuchukua maoni na kuyafanyia kazi.” Alisema Bw. Sichinga.
Bw. Sichinga alisema kuwa TCCIA inaendelea kufanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA na hivi karibuni wanatarajia kutia saini makubaliano ya utoaji Elimu kwa Mlipa Kodi kwani Wanyabiashara wengi ni wadau wa TCCIA, lengo kuu ni kuboresha ulipaji kodi kwa hiari.
“Tunataka kuona TRA ni mlezi mkubwa wa biashara yako kwa hiyo kupitia session mbalimbali ambazo TCCIA tunazifanya wadau wetu wanapata elimu”, Alisema Bw, Sichinga.
Aidha, Bw. Sichinga alibainisha majukumu mbalimbali yanayofanywa na TCCIA ikiwemo kuratibu maonesho ya biashara kwa kuwakusanya wafanyabiashara na wazalishaji mbalimbali kwa ajili ya kuonesha bidhaa zao, kuandaa safari za kimisioni za wafanyabiashara (Trade Mission), kutatua migogoro ya kibiashara, kuwawezesha wafanyabiashara wanawake katika sekta ya ujasiriamali, kuibua wafanyabiashara wapya hasa vijana walioko Vyuoni na waliomaliza Vyuo pamoja na Kuandaa Mabaraza ya Biashara kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa.
“Kwa kupitia TCCIA Tumekuwa tukiratibu utatuaji wa migogoro ya kibiashara baina ya mfanyabiashara mmoja na mwingine kabla hawajapeleka kwenye vyombo vya sheria tunataka hawa watu wawe marafiki wasiwe maadui wakudumu, tunalea wafanyabiashara wanawake kwa sababu Serikali na Dunia nzima inamwangalia mwanamke na jinsi gani ya kumkuza katika tasnia nzima ya ujasiriamali na biashara, tunalea vijana walioko chuoni na waliomaliza chuo na wanaojifunza ujasiriamali ili wawe wafanyabiashara wazuri, tunaandaa mabaraza ya biashara kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa na kero zinatatuliwa mezani.” Alifafanua Bw. Sichinga
Kongamano hili la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoa wa Mbeya lilishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo, sekta ya kilimo, biashara za usindikaji wa mazao na washauri wa kodi, ambapo walitoa maoni mbalimbali na Kuupongeza Uongozi wa TRA Mkoa wa Mbeya kwa kuwa karibu na wafanyabiashara.