Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewasisitiza Watumishi wa Umma na Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika kesho Novemba 27, 2024 Tanzania Bara.
Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo leo akiwa Ofisini kwake katika Mji wa Serikali, Mtumba, Jijini Dodoma.
Mhe. Simbachawene amesema, zoezi la kesho ni la kihistoria katika nchi yetu hivyo kila Mtanzania mwenye sifa wakiwemo Watumishi wa Umma wote ni muhimu wakashiriki katika kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
“Kwa kuwa zoezi hili ni la kikatiba, nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ninatoa rai kwa Watumishi wote wa Umma na wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu.” amesisitiza Mhe.Simbachawene
Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku ya kesho kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa watumishi wote kwenda kupiga kura.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amewasisitiza Watumishi hao kwenda kupiga kura bila kupuuza kwani ushiriki wao kwenye mambo muhimu ya kikatiba ni kutekeleza majukumu ya kiutumishi.