Na Silivia Amandius-KAGERA
Jeshi la Polisi mkoani Kagera limejidhatiti kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Novemba 27, 2024. Kupitia msaada wa serikali, jeshi hilo limepokea magari mapya matano ili kuimarisha ulinzi katika mkoa huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, amewatoa hofu wananchi, akiwataka wajitokeze kwa wingi kusikiliza sera za vyama mbalimbali wakati wa kampeni na kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi bora.
“Tumekuwa na changamoto ya vitendea kazi kwa muda mrefu, lakini serikali imetusaidia kutatua tatizo hili. Pamoja na magari haya matano, hivi karibuni pia tumepokea magari mawili mengine. Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi na maeneo yao, naomba msiwe na hofu siku ya uchaguzi,” alisema Kamanda Chatanda.
Aidha, amewahimiza wananchi kuzingatia kampeni kwa makini na kuwachagua viongozi wenye maono na uwezo wa kusukuma maendeleo mbele kwa kushirikiana na jamii.
“Uchaguzi huu ni nafasi muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi waadilifu ambao watawasaidia kufanikisha maendeleo. Amani na utulivu ni kipaumbele chetu, na Jeshi la Polisi lipo tayari kwa jukumu hili,” aliongeza.
Wananchi wa Kagera sasa wana matumaini mapya kwamba hatua hizi zitasaidia kufanikisha uchaguzi wa amani na maendeleo ya kidemokrasia katika mkoa wao.