Na Is-haka Omar, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amewataka viongozi wa chama na jumuiya wanaohusika na masuala ya uenezi,itikadi na mafunzo kwenda na wakati wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoleta tija katika ushindani wa kisiasa nchini.
Wito huo ameutoa wakati akifungua mafunzo kwa makatibu wa siasa,uenezi,itikadi,hamasa na chipukizi pamoja na elimu na malezi wa Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake ngazi za majimbo,wilaya na mikoa minne ya CCM Unguja yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Fuji Bububu Zanzibar.
Dkt.Dimwa, ameeleza kuwa viongozi hao wana jukumu kubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwani wanatakiwa kufafanua sera na miongozo,kuhamasisha,kueneza uetekelezaji wa ilani,kutoa mafunzo kwa wanachama pamoja na kujibu hoja mbalimbali za upotoshaji zinazotolewa na vyama vya upinzani kwa dhamira ya kuchafua na kuhujumu mambo mema yanayotekelezwa na Chama za serikali zake.
Alisema siasa za zama za sasa zinafanyika sana katika mitandao ya kijamii na zinasambaa kwa kasi kubwa kuliko katika majukwaa ya kisiasa ya kawaida na kwamba ni lazima viongozi hao waende sambamba na kasi hiyo katika kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi kuamini kuwa CCM ndio chama pekee chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo endelevu.
Katika maelezo yake amewasisitiza viongozi hao kuendeleza utamaduni wa kujibu hoja za wapinzani na kufafanua kwa undani utekelezaji wa ilani katika maeneo yao panapotokea jambo lolote la upotoshaji hasa kwa ngazi za majimbo,wilaya na mikoa na kuacha tabia za kusubiri kazi hizo zifanywe na ngazi za kitaifa pekee.
“Nasaha zangu kwenu fanyeni kazi kwa mujibu wa majukumu yenu jibuni hoja kwa hoja sio matusi wala ubabaishaji kwani chama chetu kinatekeleza majukumu yake kwa uhalisia zaidi kwa kila nyanja.
Tangazeni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 namna ilivyofanyika katika maeneo yenu ili wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi, ambao ndio mtaji wetu wa kisiasa waelewe ili waweze kufanya maamuzi ya kuwapigia kura za ndio wagombea wetu katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025”.alisema Dkt.Dimwa.
Kupitia hafla hiyo Dkt.Dimwa, alisisitiza viongozi hao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura kwa awamu ya pili ili kupata watu wenye sifa za kuwapigia kura wagombea wa CCM.
Aliwataka viongozi hao kuepuka makundi yasiofaa ya kutumiwa kwa maslahi binafsi na baadhi ya viongozi na wanachama ndani kwa dhamira ya kutengeneza migogoro isiyofaa ndani ya taasisi hiyo.
Pamoja na hayo alibainisha kuwa Chama Cha Mapinduzi kinahitaji wabunge,wawakilishi na madiwani imara wanaofanya kazi kwa ufanisi ya kuwahudumia na kwamba kiongozi yeyote asiyetekeleza majukumu yake chama hakitompa nafasi ya kuongozakatika uchaguzi mkuu ujao.
Alifafanua kuwa ibara ya 246 (e) katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 inaeleza umuhimu wa mafunzo ya makada na viongozi wa chama kwa kudumisha na kuandaa mafunzo ili kuendeleza na kukuza elimu ya itikadi na uzalendo kwa viongozi wa CCM.
Alisema CCM inaendelea na maandalizi ya kutekeleza ibara 5 ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 inayoelekeza kuwa ushindi wa CCM ni lazima kwa ngazi zote katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja pamoja na uchaguzi mkuu wa wa dola.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya itikadi,uenezi na mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa na kuwajengea uwezo makatibu hao wakafanye kazi zao kwa ufanisi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya upatikanaji wa ushindi mwaka 2025.
“Tunaposema hakuna mbadala wa Dk.Mwinyi 20125 tunaimanisha na sasa tunatesti mitambo yetu kwa kuandaa kimafunzo jeshi letu la kisiasa kwani mwaka mwezi octoba mwaka 2025 tunaingia katika vita ya kidemokrasia ambayo kwa tathimini zetu mpaka sasa kupitia kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani iliyofanywa na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi tuna uhakika wa kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 90”.alifafanua Mbeto.
Aliwashauri viongozi wa baadhi ya vyama vya upinzani nchini kuacha chokochoko zinazoashiria kuingiza Zanzibar katika machafuko badala yake nao watumie ruzuku wanazopata serikali kufanya maendeleo kuwepo kwa ushindaji wa kisera na kwamba maneno ya majukwaani hayana tija kwa wananchi.
Kuptia mafunzo hayo ziliwasilishwa mada nne zikiwemo mahusiano na vyombo vya habari,umuhimu wa matumuzi ya mitandao ya kijamii,wajibu na maadili ya viongozi wa Chama na Jumuiya(Maandalizi ya Daftari la kudumu la wapiga kura) na maandalizi ya Mikutano.
CAPTION
Picha no.99- NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo makatibu wa siasa,uenezi,itikadi na mafunzo pamoja na makatibu wa hamasa ngazi za majimbo,wilaya na mikoa minne ya kichama Unguja yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Fuji Bububu Zanzibar.(PICHA NA AFISI KUU YA CCM ZANZIBAR).