Na Denis Mlowe, Iringa
VIJANA vyuo vikuu mkoani Iringa ni miongoni mwa walengwa watakaonufaika na mradi wa Reproductive Equity Strategy in Tanzania (REST) unaotekelezwa na shirika la Deutsche Stiftung Weltbevolkerung (DSW) kwa kushirikiana na mashirika ya TAHEA na Alama Yangu mkoani Iringa.
Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCo) na Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI).
Mkurugenzi wa DSW Tanzania, Peter Owaga amesema mradi huu umebuniwa mahususi kusaidia vijana kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya uzazi na afya ya akili, ukatili wa kijinsia, na stadi za maisha, huku ukiwa na lengo la kuwasaidia vijana kujitegemea kiuchumi na kijamii.
Katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Sunset kuelezea malengo ya mradi huo,Owaga alisema mradi wa REST utawahusisha vijana walioko ndani na nje ya mfumo rasmi wa elimu, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutokana na changamoto nyingi zinazowakumba.
Kaimu Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Iringa, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Lidya Sospeter alisema mahusiano ya kimapenzi vyuoni yamekuwa moja ya vyanzo vikuu vya ukatili wa kijinsia unaowakumba wanafunzi wa kike.
“Hali hii mara nyingi inahusisha udhalilishaji wa kingono, shinikizo la kihisia, na wakati mwingine hata matumizi ya nguvu,” alisema.
Kwa mujibu wa ripoti za dawati hilo, Sospeter alisema matukio mengi ya ukatili vyuoni hayatolewi taarifa kutokana na woga au aibu, jambo linalochochea tatizo hilo kuendelea.
Aidha alisema changamoto za matumizi ya dawa za kulevya na pombe miongoni mwa wanafunzi zimeongeza athari kwa afya yao ya akili na ustawi wa kijamii, na hivyo kuhitaji hatua za haraka.
Ili kuimarisha juhudi za kupunguza ukatili wa kijinsia, Sospeter alisema elimu itakayotolewa kupitia REST itasaidia kuwahamasisha wanafunzi kuripoti matukio ya ukatili.
“Tunatarajia kwamba kupitia ushirikiano huu, tutapunguza au hata kumaliza kabisa ukatili wa kijinsia vyuoni. Uelimishaji utatoa mwanga kwa wahanga wa ukatili kufahamu haki zao na namna ya kupata msaada,” alisema.
Mratibu wa mradi huo, Selina Protas, alisema kwa kupitia mradi huo wanalenga kusaidia kuboresha maisha ya vijana kwa kufanya ushawishi na utetezi wa sera na mifumo inayowahusu, ili wapate fursa za kufikia ustawi wa kijamii na kiuchumi.
“Mradi huu unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa, umejikita katika kuchochea mazingira rafiki kwa vijana katika upataji wa huduma za afya ya uzazi, kupunguza ukatili wa kijinsia na changamoto ya afya ya akili, kukuza usawa wa kijinsia, na stadi za maisha ili kuliwezesha kundi hilo kujitambua na kujikwamua kiuchumi,” alisema.
Alisema kupitia mradi huo, wataanzisha klabu za afya vyuoni ambazo zitakuwa vituo vya maarifa kwa vijana.
Klabu hizi zitaongozwa na vijana waliopatiwa mafunzo maalum watakaojulikana kama ‘Vijana Vinara au champions’ watakaokuwa mabalozi wa mabadiliko katika kuhakikisha elimu ya afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia na stadi za maisha zinawafikia vijana wengi zaidi,” alisema Selina.
Alisema mradi wa REST pia unalenga kuwajengea vijana uwezo kupitia mafunzo ya ujasiriamali yatakayowawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kujitegemea badala ya kutegemea msaada wa kifedha kutoka kwa washirika wa kimapenzi, hali inayochochea ukatili wa kijinsia.
Kuhusu stadi za maisha zitakazofundishwa alisema zinalenga kuwasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, na kujenga uhusiano wenye afya.
Alisema mradi wa REST unatekelezwa katika kata nne zenye changamoto kubwa mkoani Iringa, ambazo ni Ifunda, Mseke, Kising’a, na Kihorogota kwa halmashauri ya wilaya ya Iringa na Ruaha, Makorongoni, Mkwawa, Kihesa na Mtwivilla kwa halmashauri ya manispaa ya Iringa.
Alisema kata hizi zimechaguliwa kutokana na kiwango kikubwa cha changamoto zinazowakumba vijana wa maeneo hayo, hususan katika masuala ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Frank Leonard, alisema kuwa vyombo vya habari vitakuwa na jukumu muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia kupitia machapisho na vipindi vya redio na televisheni.
“Waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuelimisha jamii kupitia ripoti na mijadala. Tunapaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu na kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia walengwa,” alisema Frank.