Na Rahma Khamis Maelezo      19/9/2024

Mkuu wa  Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amewataka madereva kwenda mwendo wa wastani  wakati wanapoendesha vyombo  vya moto ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu huyo, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuendesha kwa usalama, madereva  na makonda  wa gari za abiria wa mkoa huo,  katika  ukumbi wa Ofisi ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Othman Ali Maulid, amesema uzowefu unaonesha kuwa mwendo kasi unachangia  ajali nyingi za barabarani na kuwataka wadau hao kufuata maelekezo ya mwendo yaliyowekwa katika alama za barabarani  ili watumiaji wa  barabara wabaki kuwa salama.

Ameeleza kuwa  Serikali imeweka miundombinu ya barabara ili kuhakikisha sekta ya usafiri nchini inaimarika na kuwasihi kuitumia miundombinu hiyo kama ilivyokusudiwa pasi na kuathiri watumiaji.

“Tunapoendesha vyombo vyetu kwa mwendo wa wastani itasaidia kupunguza  ajali na endapo zitatokea hzaitakua kubwa kama itavyokua ajali ya  mwendo kasi.” alisema Mkuu huyo.

Aidha amewataka waliopatiwa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri wa elimu hiyo ili kuiweka Zanzibar katika hali ya usalama kutokana na ajali za barabarani kwa Zanzibar bila ya ajali inawezekana.

Naye Mkuu wa Kituo cha Umahiri cha Kikanda katika Usalama Barabarani,  Chuo Cha Taifa  Cha Usafishaji (NIT ), Godlisten Msomanje amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha matumizi salama ya barabara katika kuadhimisha wiki ya usalama barabarani.

Alieleza kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo kwa madereva, kufanya utafiti na kutoa ushauri elekezi ili kuhakikisha usalama wa wananchi barabarani unakuwepo muda wote.

Amesema uzowefu unaonesha kuwa tatizo la usalama  barabarani ni janga  la kitaifa hivyo elimu inahitajika zaidi ili kuondoa tatizo hilo

“tumekuja Zanzibar kutoa elimu dhidi ya usalama barabarani ili kusaidia kuweka usalama wa watumiaji wa  barabara.”  Alisema mkuu huyo

Akiwasilisha mada ya Sheria na alama za barabarani, Mhandisi  Mhonja Roheje, amesema madereva wengi wanaenda kinyume na taratibu na sharia za barabarani ikiwa ni pamoja na kuendesha bila kuwa na leseni ya udereva, kutokagua vyombo vyao kabla ya kuingia barabarani pamoja na kutofuata alama za  barabarani.

 “Iwapo utakua na leseni lakini unajaza abiria kupitia kiasi bado hujafuata sheria jambo ambalo linahatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara na kuiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusimamia  mikakati zaidi ili kukomesha  tabia za  madereva na makonda wanaofanya makosa hayo.”alisema Mhandisi huyo

Kwa upande wa madereva na makondawaliyopatiwa mafunzo hayo   wameahidi kuyafanyia kazi kwa maslahi ya watumiai wa barabara na Taifa kwa ujumla na kuziomba taasisi husika kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili kutekeleza majukuumu yao kwa ufanisi.

Mafunzo hayo yametolewa na Mamlaka ya Usalama Barabarani Zanzibar kwa kushirikiana na Chuo Cha Usafirishaji Tanzania, ikiwa ni  shamrashamra za  wiki ya nenda kwa usalama Barabarani.