Na Mwandishi wetu, Smanjiro
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa kijiji cha Engonongoi kata ya Terrat, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa miaka 30 tangu mwaka 1995 hadi mwaka 2024 Nemamiyai Shinini amelalamikia kamati ya siasi ya CCM wilaya hiyo kukata jina lake ili asigombee .
Nemamiyai ambaye pia ni mganga wa jadi (Laiboni) akizungumza na waandishi wa habari amesema alishinda kwa kupata kura 700 za maoni ya CCM ya kijiji hicho ila jina lake likakatwa kwa madai kuwa hajui kusoma wala kuandika.
Amesema baada ya kushinda jina lake liliwekewa alama nzuri kupitia vikao vya tawi na kata na kisha kupitishwa na kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya na kupewa barua ya uteuzi.
“Wakati najiandaa kwenda ofisi ya kata ya Terrat kupeleka barua ili kupata fomu za kuomba kugombea serikalini nikashangazwa kukatwa jina na mgombea wa pili kuteuliwa kugombea,” amesema.
Amesema ameongoza kijiji hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 1995 kutoka kijiji mama cha Loswaki na kufanikisha maendeleo mengi ila hivi sasa ndiyo wanakata jina lake.
“CCM Wilaya waliniita na kudai kuwa sijui kusoma wala kuandika ila nikaandika jina langu na kuwasomea mbele yao ila nikashangazwa na kukatwa jina langu,” amesema Nemamiyai.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer amedhbiitisha kukatwa jina kwa mgombea huo kutokana na kutojua kwake kusoma wala kuandika kiswahili.
Laizer amesema baada ya kubaini kuwa mgombea huyo hajui kusoma wala kuandika ikabidi wakate jina lake na kumteua aliyekuwa anafuata kwa kupata kura nyingi kwani muda wa uchaguzi umepita.
“Ni utaratibu wa chama tuu umetumika kwani kanuni na taratibu zinaeleza kuwa mgombea asiyejua kusoma na kuandika hawezi kupatiwa nafasi ya kuiwakilisha CCM,” amesema Kiria.
Amesema hivi sasa wanajipanga mara baada ya kuanza kampeni wanatarajia kufanya mkutano na kuzungumza na wanachama wa Engonongoi ili kuwaelezea hali ilivyo.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji hicho Alaice Mollel amesema ni vyema Nemamiyai apumzike kwani miaka 30 aliyoongoza inatosha anapaswa kuacha kijiti kwa mwingine.
“Kama hajui kusoma wala kuandika ni vyema akapisha wasomi wakaongoza kijiji kwani miaka 30 aliyoongoza inamtosha hii mitano haitamsaidia chochote kipya atakachofanya,” amesema.
Mkazi wa wilaya hiyo, Lekaita Lekaita amesema Nemamiyai ameongoza kijiji hicho kwa nidhamu, maadili, kutokula rushwa wala kuuza ardhi ya kijiji, ndiyo sababu anapendwa na kuchaguliwa.
“Kuna baadhi ya viongozi wa vijiji vingine hawajui kusoma wala kuandika na wameuza ardhi ya vijiji na bado tena wakapitishwa na CCM kugombea upya,” amesema Lekaita.
Mkazi mwingine wa Simanjiro, Mosses Ole Sanjiro amempa pole kwa kukatwa jina ila anapaswa kuwapisha wengine kwani kuongoza kwa miaka 30 ni muda mrefu inatosha.
“Mzee wangu pole sana uila ukiendelea utakuwa kama Museveni japo una haki ya kuongoza kama watu wanakupenda ila CCM wamekufanya mbuzi wa kafara kwani wapo viongozi wa vijiji na vitongoji hawajui kusoma wala kuandika ila wameachwa wagombee,” amesema.
Mkazi mwingine Zephania Meshaki amesema Nemamiyai ameonewa kwani wapo baadhi ya wagombea wakiwemo nafasi ya ujumbe wa serikali ya kijiji hawajui hata kiswahili ila wamepitishwa.
“Pole mzee kwa sababu chama kimekuonea kwani baadhi ya wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa serikali ya vijiji ambao hawajui lugha ya taifa wakati vikao vinaendeshwa kwa luga ya taifa chama kimekuosea umeonewa peke yako,” amesema.