NA BALTAZAR MASHAKA, ILEMELA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela imeonesha mafanikio katika ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya kwanza cha mwaka wa fedha 2024/25.
Hadi kufikia Septemba 30, 2024, halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.7 za mapato ya ndani, sawa na asilimia 25 ya lengo la makusanyo ya jumla la shilingi bilioni 14.9 kwa mwaka huu.
Aidha, shilingi bilioni 6.1 sawa na asilimia 31 ya bajeti ya miradi ya maendeleo kimepelekwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta tofauti, katika huduma za jamii hasa elimu, afya na miundombinu.
Katika taarifa aliyoiwasilisha leo mbele ya Baraza la Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu, alisisitiza mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kugawa mapato ya ndani katika sekta mbalimbali.
Amesema, shilingi milioni 317.3 zilizovuka mwaka 2023/24 zilielekezwa kulipa fidia ya ardhi, huku shilingi milioni 400 zikienda katika ujenzi wa shule mpya ya sekondari Masemele, shilingi milioni 262 zimeelekezwa kwa mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na zaidi ya milioni 140 zimetumika kukamilisha ujenzi wa wodi ya wazazi katika zahanati ya Nyakato.
Miradi mingine ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 imejumuisha ujenzi wa barabara shule,zahanati,madarasa,matundu ya vyoo,nyumba za walimu na vituo vya afya.
Wayayu pia ameeleza kuhusu ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na barabara za lami zinazojengwa kutoka Buswelu hadi Nyamhongolo na Buswelu-Busenga hadi Cocacola.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga, amewakumbusha madiwani na watendaji wa kata na mitaa kuwa ni muhimu kuweka kipaumbele katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuhakikisha maendeleo endelevu katika maeneo yao.
Pia amesisitiza umuhimu wa kutumia ardhi kwa njia bora, na alipendekeza kuachana na ujenzi wa madarasa ya kusambaa chini na badala yake kujenga ghorofa ili kukabiliana na changamoto ya ongezeko la idadi ya wakazi wa Manispaa ya Ilemela.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Wakili Mariam Msengi,amewasisitiza madiwani umuhimu wa usimamizi madhubuti wa mapato na fedha za miradi na kuhakikisha zinazopokelewa na zinatumika ipasavyo ili kuteta tija katika maendeleo ya wananchi.
Madiwani pia walikuwa na michango mbalimbali, ikiwemo ombi la Diwani wa Kiseke,Ramdhani Mwevi,amemshauri Mkurugenzi kuhakikisha eneo la zahanati ya Lubala linapata hati miliki kwa jina la halmashauri ili kuondoa changamoto za umiliki wa ardhi.