Na Ashrack Miraji, Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Japhari Kubecha, amepongeza waandaaji wa Shindano la Samia Challenge kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kuamua kufanyia shindano hilo mkoani Tanga. Akizungumza katika hafla hiyo, Kubecha alisema kuwa mkoa huo uko tayari kuandaa matukio mengine ya aina hiyo siku za usoni.
“Kwanza kabisa, nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kuwa hapa leo, tukijadili mafanikio yaliyopatikana kupitia Samia Challenge. Tumeshuhudia matokeo chanya katika sekta mbalimbali,” alisema Kubecha.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha demokrasia na diplomasia chini ya uongozi wa Rais Samia, akieleza, “Ni lazima tumshukuru Rais kwa juhudi zake za kuimarisha makundi mbalimbali, na tunajivunia maendeleo makubwa yanayoendelea nchini.”
Aidha, Kubecha alisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kulitaja jina la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na mafanikio ambayo mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla yamepata.
“Niwapongeza washindi wa Samia Challenge, waliopatikana kwa lengo la kuonyesha umahiri wa Rais katika kuleta mabadiliko. Pia, kupitia mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, tunahitaji kutazama jinsi ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kupitia asilimia 2 ya mikopo hiyo,” aliongeza Kubecha.
Alihitimisha kwa kusema kwamba juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono ili kuendeleza maendeleo endelevu katika Wilaya ya Tanga.