WANAFUNZI zaidi ya 1, 600 wa shule za sekondari mkoani Njombe wamenufaika na program ya kinadharia na vitendo kupitia klabu za kilimo na uhifadhi wa mazingira inayoendeshwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kupitia program ya Forest and Farm facility (FFF).
Hayo yalielezwa juzi na Mratibu Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoa wa Njombe, Nobert Mwalongo katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa chakula yanayofanyika katika shule ya sekondari Ninga wilayani Njombe.
Mwalongo alisema program hiyo ni sehemu muhimu katika kuendeleza na kuhimarisha maarifa ya vijana na wanafunzi katika mfumo wa chakula unaoweza kuwapa lishe bora pamoja na utunzaji wa mazingira.
“Tumegundua suala la elimu wanafunzi kujitegemea hususani katika nchi ambayo kwa upana wake imetawaliwa zaidi na wakulima hivyo tumeona ipo haja ya kushirikisha wanafunzi,” alisema Mwalongo.
Alisema Shule hizo kupitia klabu zao zimeshiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira na kilimo cha bustani za mbogamboga kwa kutumia njia za kiikolojia ambapo MVIWATA iliwezesha vifaa ikiwemo mbegu za mbogamboga, miti na vifaa vya kumwagilia (Watercane).
“Utekelezaji wa program ya uanzishaji wa klabu za kilimo na mazingira ulianza na wilaya mbili (Ludewa na Njombe) na kuzifikia shule 15 zenye jumla ya wanachama 724 Jitihada hizo za ushirikishaji wa wanafunzi umekuwa ukiendelea na sasa zimeongezeka shule tatu ikiwemo mbili katika wilaya ya Wanging’ombe na moja katika Wilaya ya Ludewa,” alisema Mwalongo.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Shule ya Sekondari Ninga, Geofrey Mgina alisema mpaka sasa shule hiyo imefanikiwa kuanzisha mradi wa matunda, miti ya biashara, mazao ya chakula pamoja na bustani ya mbogamboga ambayo imesaidia kuwaongezea kipato pamoja na lishe kwa wanafunzi.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Mendrad Nziku alizishukuru shule ambazo zimekubali kupokea mradi huo na kwamba elimu wanayoipata wanafunzi hao itawasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Baadhi ya wanafunzi akiwemo, Daniel Kifyulilo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Ninga alisema progam hiyo imewasaidia kupata elimu juu ya kuandaa bustani za mboga mboga na kuzitumia ili kuhimarisha lishe zao.