Na Mwandishi Wetu, Arusha
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi Mhe. Geophrey Pinda ameongoza harambee iliyochangisha Shilingi milioni 132 kwa ajili ya kusaidia Ujenzi wa kituo cha watoto yatima cha “The Joy of God Ophanage Center” kilichopo jijini Arusha.
Hafla ya harambee hiyo imefanyika tarehe 22 Oktoba 2024 katika nyumba ya Bushback Safari Kilenge iliyopo mtaa wa Impla jijini Arusha.
Akitoa shukurani kwa wananchi, wadau pamoja na viongozi wa serikali waliofika katika harambee hiyo Mhe. Pinda amewasihi Watanzania kujitoa kuwasaidia, kuwalea na kuwajengea makazi watoto wasio na uwezo wakiwemo yatima.
“Tutakuwa na ushahidi kwamba tuna kitu tutakifanya, hizi milioni 132 zinakwenda kusaidia watoto hawa wenye uhitaji maalumu, uhitaji maalum maana yake hawana walezi na sasa tumeamua kusaidiana na ‘Sister’ katika kuwalea, kuwanjea makazi na maisha yao kuwa salama” amesema Mhe.Pinda
Aidha, amezishukuru taasisi zote za kifedha zilizoshiriki katika harambee hiyo huku akiasa taasisi nyingine kwamba, bado zina nafasi ya kuchangia ujenzi zaidi wa kituo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Gasper Mtahengerwa amewashukuru wananchi kwa kujitolea kwa moyo wa dhati katika kuhakikisha wanafanikisha ujenzi wa kituo hicho.
“Niwashukuru sana kwa namna mlivyoguswa katika utoaji wenu hakika ni jambo la kushukuriwa mno ili kuwalea vema watoto wetu hawa” amesema Mhe. Mtahengerwa
Naye Mlezi wa kituo hicho Sister Janeth Ngopa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Naibu Waziri wa Ardhi kwa kushiriki na kuendesha zoezi hilo kikamilifu la uchangiaji ujenzi wa kituo hicho.
“Kwa niaba ya watoto wadhamini na bodi ya kituo hiki ninamuomba Mungu ampe maisha marefu Mungu, ampe afya njema na tunamuomba asichoke kutusaidia kwa sababu mara kwa mara tutamsumbua kwa njia ya simu kutusaidia” amesema Sister Janeth.
Katika kuboresha makazi ya watoto hao wasio na uwezo, kituo hicho kimeanzisha na kinaendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa mbili ambalo msingi wake umekamilika katika eneo la Gomba Estate jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akiwa amembeba mtoto wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha watoto yatima cha “The Joy of God Ophanage Center” kilichopo jijini Arusha tarehe 22 Oktoba 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kituo cha watoto yatima cha “The Joy of God Ophanage Center” kilichopo jijini Arusha tarehe 22 Oktoba 2024.
Sehemu ya washiriki wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha watoto yatima cha “The Joy of God Ophanage Center” kilichopo jijini Arusha tarehe 22 Oktoba 2024.