MABINGWA Watetezi timu ya Yanga imeendelea kuwa mbabe kwa mpinzani wake Simba Sc mara baada ya kuizamisha bao 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa aina yake, tumeshuhudia kandanda safi kutoka kwa timu zote mbele hasa kwa kucheza soka la kushambuliana kwa dhamu bila mafanikio katika kipindi cha kwanza na cha pili kabla ya Yanga kupata bao la ushindi kwenye mchezo huo.
Kipindi cha kwanza Simba ilipata nafasi ya wazi kupitia kwa mshambuliaji wake hatari Leonel Ateba lakini mlinda lango machachari wa Yanga Djidji Diara kuokoa hatari hiyo na kuwafanya kuwa salama kwenye dakika hizo.
Mpaka kipindi cha kwanza kuisha mechi ilikuwa 0-0, licha ya nafasi nyingi kutengenezwa na nyota wa timu hizo mbili.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kwa dakika kadhaa za mchezo ambapo faida ya mabadiliko ilionekana kwa Yanga kwani ilimuingiza kiungo wao mshambuliaji Chama ambaye alitengeneza shambulio la hatari ambalo lilizaa bao kupitia kwa beki wa Simba Kijiri kujifunga akijaribu kuokoa.
Kwa matokeo hayo Yanga SC wamefikisha Pointi 15 na kushika nafasi ya pili huku wakiwa wamecheza mechi tano,Simba SC anashuka mpaka nafasi ya nne akiwa na Pointi 13 akiwa amecheza mechi sita na Singida blacks Stars bado wanaongoza ligi wakiwa na pointi 16 wakiwa wamecheza mechi sita.