Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas sambamba na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius wamepita Kijiji kwa Kijiji katika tarafa ya Masasi wilayani humo wakihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kimelembe kata ya Nkomang’ombe mkuu wa wilaya ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
“Msikubali kikundi cha watu wachache kiwachagulie viongozi vijiji na vitongoji, niwaase sana ndugu zangu mjitokeze kwa wingi kwenda kujiandikisha ili mpate sifa ya kuchagua viongozi wenu”. Amesema Thomas
Aidha mkuu wa wilaya huyo ameongeza kwa kusema kuwa uchaguzi upo tangu enzi za mitume na manabii kuwa ukisoma Quran na Biblia utakutana na historia za makundi mbalimbali yaliyochagua viongozi wao na kuwaongoza hivyo changuzi hizi za Serikali za Mitaa na chaguzi nyinginezo ni mwendelezo wa tangu awali.
Aidha kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius amesema siku za kujiandikisha zimebaki chache na kuwaomba wananchi waendelee kujitokeza kujiandikisha ili waweze kupata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kwani bila kufanya hivyo hawataweza kupiga kura.
” Suala la kujiandikisha wala halichukui muda mrefu hata nusu saa haifiki, na wala hauitaji kuwa na kiambatanisho chochote, ni suala la wewe tu kwenda katika kituo na kuandikisha majina yako”. Amesema Deogratius.
Baadhi ya vijijini vya tarafa ya Masasi ambavyo ziara hiyo imefanyika ni pamoja na kijiji cha Kimelembe, Nkomang’ombe, Luilo, Kiyogo, Ngelenge na Nsungu huku wakaendelea na Vijiji vinginevyo.