Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi,amezitaka taasisi zote zilizopo katika masuala ya haki jinai nchini kuimarisha weledi katika shughuli zote za upelelezi.
Prof. Kabudi ameyasema hayo leo Oktoba 9,2024 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU).
Prof.Kabudi amezipongeza taasisi hizo kwa kazi nzuri wanazozifanya kwa kutenda haki katika masuala ya haki hivyo niziombe taasisi zote zinazohusika na haki jinai kuongeza ufanisi pamoja na weledi katika kutenda haki.
“Nawapongeza kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi hivyo nawaomba mfanye kazi kwa kufuata taratibu na sheria na kanuni za nchi ili muendelee kumsaidia Mhe.Rais Samia Suluhu katika kutekeleza majukumu ya kila siku”amesema
Aidha, amesema kuwa taasisi hizo tatu zinapaswa kufanya mambo yao kwa mujibu wa sheria,taratibu na kanuni bila ya kuathiriwa na mihemuko ya kundi au mtu fulani.
“Fanyeni mambo yenu kwa weledi semeni mambo ambayo yapo tayari kusemwa kwa umma lakini kama jambo bado lipo kwenye uchunguzi endeleni kufanya uchunguzi bila kuathiriwa na kitu ama mtu yoyote yule”amesisitiza Prof.Kabudi
Vile vile, amewataka kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara ili kufahamia na kila mmoja kujua majukumu yake yanaishia wapi na ya mwenzake yanaanzia wapi ili kurahisisha uendeshaji wa mashauri na kutoa haki kwa wakati.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwakani Prof. Kabudi, ameziagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,TAKUKURU na Ofisi ya Upelelezi wa makosa ya Jinai kusimamia sheria ili uchaguzi huo uwe huru na wa haki.
“Navitaka vyombo vya upelelezi nchini kuhakikisha vinazingatia sheria na haki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu na uchaguzi Mkuu mwakani ili kudumisha umoja, amani na usalama wa nchi.”amesisitiza Prof.Kabudi
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Slyvester Mwakitalu, amesema kikao hicho ambacho kinakutanisha ofisi zinazounda utatu katika masuala ya haki jinai nchini lengo lake ni kujadili changamoto mbalimbali katika sekta hiyo pamoja na kuandaa mikakati ya kupata suluhu.
“Umoja wetu huu unajulikana kama Utatu lengo la kikao hichi ni hizi taasisi zetu tatu kukutana na kujadilina mambo mbalimbali ikiwemo changamoto zilizopo ambazo kwa namna moja au nyingine zinawanyika haki wananchi, kufanya tathimini ya mwaka mzima na kuweka mikakati ya mwaka ujao”amesema Mwakitalu