Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Chacha wakati alipowasili Wilaya ya Igunga katika kuanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora leo tarehe 08 Oktoba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Igunga wakati akianza Ziara ya Kikazi mkoani Tabora leo tarehe 08 Oktoba 2024.
………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 08 Oktoba 2024 ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora.
Ziara ya Makamu wa Rais imeanzia Wilaya ya Igunga ambapo amezungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika eneo la barabara ya Mwanzugi wilayani humo.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Igunga kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa wazalishaji wazuri na muhimu wa mazao ya chakula,biashara pamoja na ufugaji. Amesema serikali itaendelea kuboresha huduma za kijamii katika Wilaya hiyo zikiwemo huduma za maji, elimu, afya na miundombinu ili kurahisisha shuguli za kiuchumi wilayani humo.
Makamu wa Rais ameiagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kushughulikia ujenzi wa soko la kisasa na kituo cha mabasi cha Wilaya ya Igunga kutokana na mahitajio ya wananchi. Pia amesema kutokana na upungufu wa watumishi katika katika sekta mbalimbali wilayani humo, TAMISEMI inapaswa kutoa kipaumbele kwa wilaya hiyo wakati wa upangaji wa watumishi.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa maeneo hayo kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata elimu mashuleni badala ya kuwaruhusu kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini migodini.
Vilevile Makamu wa Rais amewataka viongozi hususani wabunge wa maeneo hayo kuendelea kutoa elimu na hamasa ya mitungi ya gesi ili kwa wananchi ili kuchagiza azma ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la uhifadhi wa mazingira na afya za wananchi.
Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Igunga kujitokeza katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2024 ili kuchagua viongozi bora watakaoshirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema serikali itaendelea kumlinda mkulima kwa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao yanayolimwa wilayani humo na maeneo mengineyo ikiwemo mazao jamii ya mikunde kama vile mbaazi, choroko na dengu. Amesema lengo la kuanzisha mfumo huo ni kuondokana na d madalali ambao hununua mazao kwa bei ya chini zaidi ya soko.