MSAIDIZI wa mama lishe soko la samaki Malindi, Khadija Nassor, akitoa maoni yake juu ya kutumikishwa kwa watoto wakati Tume ya haki za binaadamu na utawala bora ikichukua maoni ya wadau kuelekea kuandaa mpangokazi wa Kitaifa wa haki za binaadamu na Biashara.

SHEHA wa Shehia ya Malindi, akitoa maoni yake juu ya kutumikishwa kwa watoto wakati Tume ya haki za binaadamu na utawala bora ikikusanyaji maoni ya wadau kuelekea kuandaa mpangokazi wa Kitaifa wa haki za binaadamu na Biashara. 

(PICHA NA FAUZIA MUSSA).

NA FAUZIA MUSSA

WAFANYABIASHA na wadau wa uchumi wa buluu wameishauri  Tume ya haki za Binaadamu na utawala bora (THBUB), kulipa uzito suala la utumikishwaji wa watoto wakati wa kuandaa Mpango kazi wa haki za binaadamu na Biashara  ili kukomesha vitendo hivyo  kwa  maslahi ya watoto na maendeleo ya Taifa.

Wadau hao walitoa rai hiyo  katika soko la samaki Malindi Mjini Unguja, wakati wakitoa maoni yao kwa Tume hiyo  ikiwa ni awamu ya  pili  ya kuchukua maoni ya wadau katika maandalizi ya mpangokazi wa Kitaifa wa haki za binaadamu na biashara.

Walisema licha ya kuwa katika soko hilo  hakuna utumikishwaji wa watoto  unaonekana lakini bado baadhi ya maeneo matukio kama hayo yapo  na yanaendelea kuwaathiri watoto na taifa.

“uzowefu unaonesha  kuwa  watoto  wengi  wanaotumikishwa  huacha  kabisa masomo yao na  wanaoendelea hupata matokeo mabaya katika masomo yao, hali hii itatupelekea kuwa na  Vijana tegemezi ndani ya jamii kama halikudhibitiwa. ” walisema wadau hao

Waliongeza kwa kusema kuwa hali  hiyo inasababishwa na baadhi ya watoto hao kuishi karibu na maeneo ya bahari  pamoja na  haliduni za maisha  kwa baadhi ya jamii na familia zao.

Aidha walieleza kuwa malezi ya mzazi mmoja hasa yanayosababishwa   na kuachana kwa wazazi hao kunachangia baadhi ya watoto kujiingiza katika biashara kinyume na sheria.

” watoto hawa  huingia katika biashara kwa sababu ya wazazi au walezi   kukosa kipato cha kuwahudumia ipasavyo hali inayowasukuma kuanza kujipanga kupambana na maisha kutokana na kuona  familia zao hazina  uwezo wa kukidhi mahitaji  ya sasa na hata baadae.” alisema msaidizi wa mama lishe soko la samaki Malindi Khadija Nassor.

Hivyo aliishauri  Tume ya haki za binaadamu na Utawala Bora kutoa elimu Kwa jamii juu ya Athari za  utumikishwaji wa watoto na kuwaomba wazazi kutopeana talaka kiholela, pamoja na kuchukua juhudi za  kutimiza mahitaji ya watoto  ili kuwapa fursa ya kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu.

Kwaupaande wake Naibu Katibu mtendaji tume hiyo Ofisi ya Zanzibar Juma Msafiri Karibona alisema wakati tume hiyo ikiandaa  Mpango kazi huo itazingatia maoni  yaliyotolewa na wadau ili kupata Mpangokazi uliozingatia  maslahi ya jamii.

Alifahamisha kuwa katika kuandaa mpangokazi huo watahakikisha wanawafikia wadau wote waliokusudiwa ili kupata mpango shirikishi  kwa maslahi ya Taifa.

katika kupata maoni juu ya utumikishwaji wa watoto tume hiyo ilikutana na wafanyabiashara na wadau wa uchumi wa buluu  katika soko la samaki ngalawa, malindi  na fumba kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na kuchukuwa maoni  katika maeneo ya wadau kama  hao  walio katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja.