Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa tarehe 27 Novemba, 2024 ili kuchagua viongozi bora.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akitoa Maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 kwa waandishi wa habari ofisini kwake leo tarehe 26 Septemba, 2024.
Dkt. Sagamiko alisema “niwahamasishe wananchi wa halmashauri ya jiji la Dodoma kujitoleza kwa wingi siku ya uchaguzi ambayo ni jumatano ya tarehe 27 Novemba, 2024 ili kuchagua viongozi bora watakaoongoza”.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema kuwa wananchi wenye sifa za kushiriki wanatakiwa kushiriki. “Ninatoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa uchaguzi, kuanzia hatua ya kujiandikisha kwenye orodha ya mpiga kura. Kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ni hatua inayompa kila mwananchi mwenye sifa haki ya kisheria kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea nafasi ya uongozi” alisema Dkt. Sagamiko.
Akiongelea nafasi zitakazogombewa alizitaja kuwa ni mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa kamati ya mtaa mchanganyiko na kundi la wanawake. “hivyo, wananchi wenye sifa wanahimizwa kuchukua na kurudisha fomu za kugombea nafasi hizo kwa tarehe zilizoainishwa katika maelekezo haya. Ushiriki wa wananchi wengi katika kugombea nafasi hizi ni muhimu katika kukuza demokrasia na kuhakikisha upatikanaji wa viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma alitoa maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 mbele ya waandishi wa habari, viongozi wa vyama vya siasa na makundi maalum pamoja na wadau wengine.