Walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wametakiwa kuongeza juhudi katika kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja la nne, ambalo limekuwa kikwazo kwao kuendelea na masomo katika vyuo vya kati.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohammed Gombati, alitoa wito huu wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa shule za sekondari zilizofanya vizuri mwaka 2023. Ambapo Aliwataka walimu kuhakikisha wanafunzi wanaofaulu kwa kupata madaraja ya chini, kama daraja la nne, wanapungua ili kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na vyuo vya kati.
“Ni jukumu letu kama walimu kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi unakuwa bora zaidi, na kupunguza idadi ya wale wanaopata madaraja ya chini. Hii itasaidia kuwa na wanafunzi wengi zaidi wanaoweza kuendelea na masomo ya juu katika vyuo vya kati,” alisema Mohammed Gombati.
Katika kipindi cha mwaka 2022-2023, jumla ya shule za sekondari 29 zimeanzishwa katika Wilaya ya Geita, hatua iliyochangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi. Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Geita, Hossana Nshulo, alieleza kuwa ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kutoka asilimia 82 mwaka jana hadi asilimia 87 mwaka huu, akionyesha kuwa kuna maendeleo makubwa yaliyopatikana.
“Kuanzishwa kwa shule hizi mpya kumekuwa na athari kubwa chanya katika ufaulu wa wanafunzi wetu. Tunajivunia kuona ufaulu ukiongezeka mwaka hadi mwaka,” alisema Hossana Nshulo.
Walimu walioshiriki kwenye hafla hiyo pia walitoa maoni yao, wakiiomba serikali kuendelea kuwapa motisha ili kuimarisha ari yao ya kufundisha. Walimu hao walisema kuwa motisha ni muhimu kwao kwani inawapa nguvu ya kuendelea kufundisha kwa bidii, jambo linaloleta matokeo bora kwa wanafunzi.
Angel Mfugale, mwalimu wa Shule ya Sekondari Magenge, alisisitiza umuhimu wa walimu kupewa motisha zaidi ili kusaidia wanafunzi kufikia malengo yao ya kielimu.
Patrick Ntayembala, mwalimu wa Shule ya Sekondari Bugarama, aliongeza kuwa walimu wanapaswa kutumia mbinu bora za ufundishaji huku wakipata msaada wa serikali kwa vifaa na motisha muhimu.
Wito huo unalenga kuboresha elimu katika Wilaya ya Geita na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata nafasi zaidi za kujiendeleza kielimu na kitaaluma.