📍 Dodoma
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kuongeza ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja na wadau wengine ili kupata fedha zinazohitajika kukamilisha miradi ya maji katika vijiji 1,575 ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo nchini.
Ushauri huo umetolewa Septemba 9, 2026 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na mlezi wa RUWASA, Bi. Rose Ambrose, wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti pamoja na Mameneja wa RUWASA wa Mikoa na Wilaya.
Amesema kuwa RUWASA inakabiliwa na mahitaji ya Sh trilioni 5.1 kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vilivyosalia, wakati fedha zilizopo ni Sh trilioni 2.06, hivyo kuna pengo la takribani Sh trilioni 3.
Aidha,Bi. Rose amebainisha kuwa upatikanaji wa fedha hizo unahitaji mikakati mipya, ikiwemo kushirikisha Sekta Binafsi na wadau wengine, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji.
Pia ameongeza kuwa RUWASA tayari imefanikisha kuwafikishia huduma ya maji zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wanaoishi vijijini, hivyo hatua inayofuata ni kuhakikisha vijiji vyote vilivyobaki vinafikiwa na huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Ruth Koya, amesema utekelezaji wa jukumu hilo unaendana na azma ya Serikali ya kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wanawake ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Wolta Kirita, amesema katika kuongeza kasi ya huduma hiyo, wakala huo umepanga kuanzisha miradi mipya 400 kutoka mpango wa awali wa miradi 314, huku ukilenga pia kukamilisha miundombinu ya maji 858 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Ameongeza kuwa kikao kazi hicho kitajadili mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na namna ya kupata vyanzo mbadala vya fedha, hatua inayolenga kupunguza zaidi idadi ya vijiji ambavyo bado havina huduma ya maji.

