Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Twende,John Rexford Nzira akizungumza katika maadhimisho hayo mkoani Arusha .
Mwenyekiti wa bodi ya TEN/MET ,Faraja Nyalandu akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika ofisi za Taasisi hiyo mkoani Arusha .
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .TAASISI isiyo ya kiserikali ya Twende inayowajengea watanzania uwezo wa kubuni teknolojia mbalimbali zinazotumika kutatua changamoto za kila siku imetoa mafunzo ya ubunifu wa teknolojia kwa zaidi ya Wanafunzi Elfu tano kutoka mikoa ya Arusha ,Kilimanjaro,na Manyara .
Aidha Taasisi hiyo imetoa mafunzo kwa wanafunzi hao kuhusu maswala ya ubunifu wa teknolojia na ujasiriamali ambapo wameweza kubuni mashine mbalimbali za ubunifu wakisaidiwa na wataalamu kutoka taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Twende,John Rexford Nzira ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya mafunzo ya ubunifu kwa wanafunzi .
John amesema kuwa, Taasisi hiyo ina zaidi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ,ambapo imekuwa ikitoa mafunzo sio kwa wanafunzi tu bali kwa wanajamii wote kuhusu maswala ya ubunifu ambapo imekuwa na mchango mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii kwa kubuni mashine mbalimbali .
“Leo tunaadhimisha miaka 10 ya mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambapo wataalamu wetu hutembelea mashuleni na kuweza kusikiliza mawazo ya wanafunzi na kuwajengea uwezo wa ubunifu kulingana na wazo lao ambapo wamekuwa wakifanya kazi na wanafunzi zaidi ya 500 hadi 700 kwa mwaka .”amesema .
John amesema kuwa, lengo la kuwafikia wanafunzi hao ni ili kuwawezesha kuwa wabunifu wakiwa tangu wadogo kulingana na hali.ya maisha ya sasa hivi kwani kupitia bunifu hizo wataweza kujiajiri wenyewe .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya TEN/MET ,Faraja Nyalandu amepongeza kitendo hicho kilichofanywa na taasisi hiyo kwani kinasaidia sana wanafunzi kuwa wabunifu na kuweza kuja na miradi mbalimbali ya kutatua changamoto kwenye jamii pindi wanaohitimu masomo yao.
“Hapa tumeona namna ambavyo wanafunzi wameonyesha bunifu mbalimbali walizoweza kubuni kwa kuwezeshwa na taasisi hii kwa kweli ni kitu kizuri sana katika sekta ya elimu na kinapaswa kuigwa na wengine kwani kwa dunia ya sasa hivi tunahitaji zaidi wabunifu katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.”amesema Faraja.
Kwa upande wa wanafunzi walionufaika na Taasisi hiyo, Julieth Marco na Haruna Miraji wamesema kuwa, taasisi hiyo imewasaidia sana wao kuwa wabunifu kwa kubuni mashine mbalimbali ambazo zina uwezo mkubwa wa kutatua changamoto katika jamii inayowakabili.
“Kwa mfano mimi nimeweza kupata elimu ya ubunifu kuhusu vitu vipya na kuweza kutengeneza mashine mbalimbali kama hii ya kuchuja maji machafu ambayo nimetengeneza na itasaidia sana kuokoa uchafuzi wa mazingira kwenye jamii hivyo hili ni jambo la kuigwa na taasisi mbalimbali .”amesema .