NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
AKINAMAMA 100 wajawazito wilayani Nyamagana, Jijibla Mwanaz wamenufaika na msaada wa vifaa vya uzazi vyenye thamani ya shilingi milioni 5, vilivyotolewa na The Desk & Chair Foundation.
Msaada huu unajumuisha pia ujenzi wa shimo la kisasa la kuhifadhi kondo la nyuma (placenta pit) katika Kituo cha Afya Makongoro, lililogharimu shilingi milioni 5.4, lengo likiwa ni kuboresha huduma za uzazi katika eneo hilo linalohudumia kata tatu,zikiwemo za wilaya za Sengerema na Misungwi.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee, leo amesema taasisi hiyo imekamilisha ujenzi wa shimo hilo kwa ubora wa juu na kukabidhi mradi huo kwa uongozi wa kituo hicho.
Amesema msaada huo unatolewa katika kipindi ambacho Waislamu duniani wanasherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), hivyo ni furaha kutoa vifaa hivyo muhimu kwa akina mama wajawazito.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makongoro, Dr. Emma Maneno, ameleza kuwa ujenzi wa shimo hilo utaboresha usafi na mazingira katika kituo hicho, hasa katika huduma za afya ya uzazi, amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira safi kwa wahudumu na wagonjwa.
Amesema kituo hicho kinahudumia zaidi ya watu 25,000 kwa mwaka, kwa siku kina hudumia watu 250 hadi 300, kina uhaba wa viti 30 (mabenchi) , kompyuta, vifaa vya matibabu, miundombinu ya umeme, umeme wa dharura na mashine ya alama za vidolle (Biometric Scaner).
Diwani wa Mirongo, Hamidu Seleman, alitoa shukrani kwa The Desk & Chair Foundation kwa msaada huo ambao unalenga kuboresha usalama wa akina mama na watoto na kuhimiwahimiza wadau kuendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za afya.
Kwa mujibu wa Diwani huyo wa Mirongo , serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma na miundombinu ya kituo hicho .
Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dr. Furaha Mwakafwila, amesisitiza umuhimu wa kutumia vituo vya afya kwa ajili ya uzazi salama na kuhimiza akina mama kupeleka watoto kliniki kwa chanjo.
Amesema atashangaa kuona akinamama wajawazito wakiendelea kujifungulia nyumbani ama njiani ilhali serikali imeendelea kuboresha huduma , miundombinu,dawa na vifaa tiba kuhakikisha wanapata wananchi huduma bora za matibabu.
Akina mama walionufaika kwa niaba ya wenzao Rebecca Chacha na Jacky Anthony, walishukuru kwa msaada huo, wakisema unawasaidia kupunguza gharama za kujifungua na kuimarisha usalama wa watoto wao.
Awali Sheikh wa Bilal Muslimu Kanda Ziwa, Sheikh Hashimu Ramadhan amesema Mtume Muhammad S.W.A, aliletwa kuwa huruma na rehema kwa viumbe vyote,kazi kubwa aliyoifanya kuja kukamilisha tabia nzuri inayotutaka kujenga upendo, ushirikiano na amani pomoja na viumbe wengine aliletwa kuwa suluhu ya matatizo ya wanadamu.
” The Desk & Chair Foundation wanajitolea kuihudumia jamii kwa mahitaji yao,kazi iliyokuwa ikifanywa na Mtume, na ndio misaada hii kwa ajili ya wazazi wa kituo hiki cha afya,wanahitaji baraka na huruma akinamama ili kujifungua salama,”amesema.