Kiasi cha shilingi milioni 739 kimetumika kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kata ya Nyamanoro jimbo la Ilemela ikiwemo miradi ya elimu msingi milioni 80, elimu sekondari milioni 100 na barabara zaidi ya milioni 600
Hayo yamebainishwa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa muendelezo wa ziara yake jimboni kwaajili ya kusikiliza kero za wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki wa uchaguzi wa serikali za mtaa, kujiandikisha katika daftari la mkaazi na kilele cha mbio za Mwenge katika viwanja vya mtaa wa Mnyapala ambapo amewataka wananchi wa kata hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za miradi ya maendeleo
‘.. Tuna kila sababu ya kusema ahsante Dkt Samia, ametoa fedha nyingi sana kwaajili ya miradi ya maendeleo, Ilemela kama jimbo tumeendelea kunufaika na fedha za miradi mbalimbali na hata nyie Nyamanoro mmenufaika pia, miradi mikubwa inaendelea kutekelezwa, barabara nyingi zinaenda kufunguliwa ndani ya kata yenu ..; Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea na kasi ya kukamilisha miradi mikubwa na ya kimkakati ikiwemo reli ya mwendo kasi na kisasa ya SGR, daraja la Busisi, meli kubwa za MV Mwanza Hapa Kazi Tu, upanuzi wa uwanja wa ndege Mwanza na miradi mikubwa ya maji hivyo kuwaasa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuharakisha maendeleo
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamanoro Mhe George Maganiko Ngaka mbali na kuishukuru serikali kwa fedha za miradi ya maendeleo amempongeza mbunge huyo kwa kuchochea shughuli za maendeleo ndani ya kata yake pamoja na kuahidi kuendelea kushirikiana nae ili kuwaletea maendeleo wananchi wake
Jeremiah Lugembe ni mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela akijibu maswali yaliyoulizwa na wananchi wa kata hiyo amesema kuwa manispaa ya Ilemela itaendelea kutenga fedha za mapato ya ndani na serikali kuu kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya kata hiyo ikiwemo elimu na afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kutatua kero za wananchi
Nae Joachim Elias na Anna Samuel ni wananchi wa kata ya Nyamanoro kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi ndani ya kata yao huku wakitaka barabara za mitaa ya kata hiyo kurekebisha ili kuwaondolea kina mama wajawazito adha wakati wa kujifungua
Mbunge wa Jimbo la Ilemela amehitimisha ziara zake kwa awamu ya pili akiambatana na wataalam wa manispaa ya Ilemela na wakuu wa taasisi zinazofanya kazi ndani ya wilaya hiyo ikiwemo Tanesco, MWAUWASA na TARURA mkazo ukiwa ni wananchi kuendelea kuchangia na kushiriki katika juhudi za Serikali za kuleta maendeleo