Wananchi wa jimbo la Ilemela mkoani Mwanza wamehamasishwa kujitokeza na kujiandikisha katika daftari la mkaazi katika maeneo wanayoishi ili waweze kupiga kura za kuchagua viongozi wao wa serikali za mtaa
Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo kwa kata za Nyakato na Kahama ambapo amesema kuwa uandikishaji wa daftari la mkaazi ni tofauti na lile la maboresho ya mpiga kura la tume huru ya taifa ya uchaguzi hivyo kuwaasa kutumia fursa kujitokeza kujiandikisha ili waweze kushiriki uchaguzi wa serikali za mtaa kwa kuchagua na kuchaguliwa
‘.. Uandikishaji wa daftari la mkazi katika mitaa yetu utaanza Oktoba 11 hadi 20, tuna wiki moja tu la watu kufanya zoezi hili na uandikishaji huu ni tofauti na ule wa uboreshaji wa daftari la kura ambao tuna vitambulisho vya tume, vitambulisho vile tutavitumia mwakani, uchaguzi huu wa serikali za mitaa unaanza na kujiandikisha katika daftari la orodha ya wakaazi wa mtaa husika ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula mbali na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo amewaomba wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika mbio za Mwenge wa Uhuru zitakapofika ndani ya wilaya hiyo siku ya mwezi Oktoba 13, pamoja na kushiriki sherehe za kilele cha kuhitimisha mbio hizo shughuli itakayofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba Oktoba 14
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyakato Mhe Jonathan Mkumba na diwani wa kata ya Kahama Mhe Samwel Buchenja kwa nyakati tofauti wameishukuru serikali kwa fedha za miradi ya maendeleo huku wakimpongeza mbunge Dkt Angeline Mabula kwa michango yake binafsi na jithada za kuchochea utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao
Mbunge Dkt Angeline Mabula yupo jimboni kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka wa 2024 uliobebwa na kauli mbiu ya ‘Serikali za mitaa, Sauti ya wananchi , Jitokeze kushiriki uchaguzi’ na mbio za Mwenge kwa wilaya ya Ilemela na kilele chake akimbatana na wakuu wa taasisi zinazofanya kazi ndani ya jimbo hilo zikiwemo Tanesco, Tarura na Mwauwasa huku akifanikiwa kuzungumza na wananchi wa kata ya Nyakato na Kahama, kufungua ofisi ya kanda ya waendesha boda boda Kangae-Nyakato-Mecco na kufunga mafunzo ya waendesha pikipiki ukumbi wa Bundersliga Nyasaka yaliyofadhiliwa na yeye mwenyewe kwa kushirikiana na chuo cha Kirumba Technical