OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hadi sasa kuna Shule za Msingi 68 za Mchepuo wa Kingereza za serikali zilizoanzishwa kwa lengo la kusaidia watoto na wazazi wenye uhitaji wa shule hizo kwa gharama nafuu.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya awali kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua Shule ya Msingi ya mchepuo wa Kingereza ya Chifu Zulu iliyoko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Septemba 24, 2024 ambayo imejengwa kwa gharama ya Sh. Milioni 626.4.
Amesema Manispaa ya Songea kutoka katika mapato yake ya ndani wameweza kutenga na kutumia fedha hiyo kujenga yenye vyumba madarasa ya msingi 12, madarasa ya wanafunzi wa awali 4, Jengo la Utawala moja , matundu ya vyoo 20 pamoja na Chumba cha TEHAMA.
Mhe. Mchengerwa amesema Shule hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia watoto na wazazi wanaohitaji huduma ya shule bora yenye mchepuo wa Kingereza kwa gharama nafuu zaidi na pia inatoa elimu ya TEHAMA kwa vitendo na inafundisha somo la Kifaransa ili kuendana na soko la dunia katika ajira na mawasiliano.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi wa awali na Msingi 491 ambao wanafundishwa mchepuo wa lugha ya kingereza isipokuwa kwa somo la Kiswahili na ilibuniwa na Halmashauri ya Manispaa hiyo kupitia Baraza la Madiwani ili kukidhi mahitaji makubwa ya shule za mchepuo huo.