Na Takdir Ali. Maelezo.
Kamanda Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Komodoo Azana Hassan Msingiri amezitaka madrsa za Dini ya Kiislamu nchini kuandaa utaratibu wa kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii ili kupata fadhila za Mwenyezi Mungu.
Ameyasema hayo wakati aliposhiriki katika zoezi la usafi wa mazingira na uchangiaji wa damu salama katika Madrassat Swiffat Nnabawiyatil Karimah (Msolopa) iliopo Kilimani Wilaya ya Mjini, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra ya kuadhimisha wiki ya madrsa hiyo.
Amesema kikosi hicho kipo tayari kushirikiana na madrsa zilioamua kuisaidia jamii sambamba na kuziomba madrsa nyengine kuiga mfano unaofanywa na madarsatul-Swiffat Nnabawiyatil Karimah (Msolopa).
‘‘Jambo lililofanywa na Madrsa hii ni zuri, na ninaziomba madrsa nyengine kuweka utaratibu wa kuwa karibu na jamii ili kujenga Umoja, Upendo na Mshikamano alisema Komodoo Msingiri.
Mbali na hayo amesema kujitoa katika mambo ya kheri ni kujitengenezea Akhera yako pale unapotanguliza na nia njema.
Kwa upande wake Faki Ussi Faki ambae ni Mkuu wa sehemu ya Uchangiaji damu mpango wa Taifa wa Damu salama amesema katika Hospitali kumekuwa na uhitaji Mkubwa wa damu na kuwashukuru waliojitokeza kuuchangia kwani itaweza kusaidia kwa kiasi Fulani.
Vile vile amewashajihisha watu wajitokeze sehemu mbalimbali kama vile Hospitali za Wilaya na katika Makao Makuu Sebleni.
Akitoa neno la Shukrani Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini katika Madrassa hio ya Msolopa Sheikh Abdallah Zubeir Marzouk amewashukuru walioshiriki katika zoezi hilo na kuwaomba kuzidisha juhudi kwani uendeshaji wa madrsa hiyo unahitaji mashirikiano ya pamoja.