📌 Aahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Wananchi.
📌 Amshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kumuamini na kumpa nafasi na fursa ya kutumikia jamii.
Na WMJJWM-DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametunukiwa Tuzo maalum na Taasisi ya Jamii Forums kama kiongozi anayepokea maoni ya wananchi na kuyafanyia kazi kupitia majukwaa ya kidijitali.
Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi hiyo Septemba 21 jijini Dar Es Salaam katika tukio la kuwatunikiwa wadau wa Jamii Forums walioandika *’Stories of Change’* zitakazoleta mabadiliko katika jamii .
Aidha Waziri Dkt. Gwajima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan aliyemuamini na kumpa nafasi na fursa ya kutumikia jamii kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Vilevile, Waziri Dkt. Gwajima amesema Tuzo hiyo imechangiwa watumishi wake wote wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na na wale wa Wizara za kisekta ambao hupokea na kuyafanyia kazi maelekezo yake kufuatia maoni na hoja za wananchi ambazo amekuwa akizipokea kutoka kwenye Jukwaa la Jamii Forums.
“Heshima hii iende kwa familia yangu na mume wangu mpenzi Advocate Gwajima ambaye, amekuwa akinipa ushirikiano mkubwa wakati wote wa kutumia hata muda wa familia kwa ajili ya kufuatilia hoja za wananchi kwenye Jukwaa hili.” amesema Waziri Dkt. Gwajima
Pia ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Wananchi kwa nafasi yake, na kuhakikisha sauti zote za wananchi zinasikilizwa na kufanyiwa kazi kadri inavyowezekana.
Amesisitiza kila mmoja ana nafasi muhimu katika mchakato wa uamuzi, na ni wajibu wa kila mmoja kama viongozi kusikiliza na kujibu yote yale yanayohitaji majibu kwa wananchi kwani tunapofanya kazi pamoja, tunafanikisha kuchochea maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Ningependa kutoa shukrani za pekee kwa Jamii Forums na watanzania kwa ujumla kwa utambuzi huu. Majukwaa kama Jamii Forums ni muhimu kwa ajili ya kuleta uwazi na ushirikiano, na ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana katika kujenga jamii bora zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jamii Forums Maxence Melo ameishukuru Serikali na wadau wengine kwa kuendelea kushirikiana na Jukwaa la Jamii Forums kujibu na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika Sekta mbali nchini kwani Jukwaa hilo limesaidia kuleta suluhu kwa changamoto za wananchi kwa kuoatiwa majibu au utatuzi na Serikali.