Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza na watumishi wa TAKUKURU leo mara baada kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akipata maelezo kutoka kwa Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega… mara baada kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai (kushoto).
Muonekano wa sehemu ya nje ya Ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora mara baada ya kukamilika kwake
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akiwa kwenye picha ya pamoja na Watumishi wa TAKUKURU mara baada kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.
…….
Na. Lusungu Helela-Tabora
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa mfano kwa kujipambanua kutenda haki na kuonesha uadilifu katika jamii huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa Mtumishi yeyote wa TAKUKURU atakayebainika kuwa sio muadilifu
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora uliogharimu kiasi cha Sh. Milioni 314.2 hadi kukamilika kwake.
Amesema TAKUKURU ni chombo kinachohitaji watumishi wenye uadilifu wa hali ya juu hivyo kwa Mtumishi yeyote ambaye sio muadilifu TAKUKURU si mahali sahihi kwa yeye kufanya kazi
Amesema ni jambo lisilokubalika kwa chombo hicho nyeti cha kuzuia rushwa halafu kukawa na Watumishi mabingwa wa kupokea.
Akizungumzia ujenzi wa ofisi hizo, Mhe. Sangu ameipongeza TAKUKURU kwa kuonesha mfano namna fedha za Watanzania zinavyotakiwa kutumika kwani thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa ofisi hizo unaonekana.
‘‘ TAKUKURU ni chombo kinachosimamia uadilifu na kinatakiwa kiwe cha kwanza kuonesha uadilifu kwa matendo yake, kwa namna nilivyokagua jengo hili nimeridhishwa mno naamini wateja wetu watakaokuja hapa kwa ajili ya kuchunguzwa hili jengo litumike kama mfano kwa kuonesha thamani ya fedha iliyotumika, niwapongeze sana kwa jambo kubwa mlilolifanya hapa’’ amesisitiza Mhe. Sangu
Hata hivyo, Mhe. Sangu ameiagiza TAKUKURU kuhakikisha inahamia katika ofisi hizo za kisasa ndani ya mwezi huu ikizingatiwa kuwa ofisi wanazozitumia kwa sasa katika Wilaya hiyo kodi yake ya pango itafikia ukomo mwezi huu.
Amesema kukamilika kwa Ofisi hizo kunaonesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha TAKUKURU inawajibika ipasavyo kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Sangu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kukubali kutoa fedha hizo ili kuhakikisha Watumishi wa Takukuru katika Wilaya ya Nzega wanatimiza wajibu wao kwa kufanya kazi katika Ofisi za kisasa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu ameitaka TAKUKURU kuzifanyia kazi kwa wakati nyaraka za mikataba ya miradi ya maendeleo ambazo huwasilishwa kwao kutoka kwa Wateja wao
Amesema kama jambo limekamilika au halina uchunguzi wowote ni muhimu nyaraka hizo zikarudishwa haraka kwa wahusika badala ya kukaa nazo kwa kipindi cha muda mrefu kwani lengo la TAKUKURU kupewa nyaraka hizo ni kuzuia rushwa ili kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inapoanza kutekelezwa isiharibike
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa nyaraka hizo za mikataba kufanyiwa kazi ipasanyo ili kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuonesha thamani ya fedha.