Waziri wa MajI Juma Aweso,akifungua koki kwenye moja ya vituo vya uchotea maji katika kijiji cha Kizuka wilayani Songea,baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),wa pili kulia meneja wa Ruwasa wilayani Songea Mathias Charles.
Na Mwandishi Wetu,Songea
WANANCHI zaidi ya 6,000 wa kijiji cha Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,wanatarajia kuondokana na adha ya huduma ya maji safi na salama baada ya Serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kuwa hatua za mwisho kukamilisha mradi wa maji ya bomba.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mathias Panglas alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2022 na ulitarajia kukamilika mwaka 2023 lakini kutokana na changamoto mbalimbali umeshindwa kukamilika kwa muda uliopangwa.
Alisema,mradi wa maji Kizuka unatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya RJ Mussa Contruction Co Ltd kwa gharama ya Sh.milioni 730,430,012.76 na chanzo chake ni kisima chenye urefu wa mita 115 na kina uwezo wa kuzalisha lita 324,000 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ni lita 227,000.
Alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kusukuma maji, ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000,ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji,kuchimba mtaro.
Kwa mujibu wa Panglasi, kazi nyingine ni kulaza,kuunganisha bomba umbali wa kilometa 10.138,ununuzi na ufungaji wa pampu na kuunganisha umeme kwenda kwenye nyumba ya mitambo.
Waziri wa maji Juma Aweso,amempongeza mkandarasi kwa kazi nzuri,lakini amemtaka kukamilisha kazi haraka ili wananchi waanze kupata huduma ya maji kwenye maeneo yao.
Alisema,huo ni mradi mkubwa unaokwenda kumaliza kabisa kero ya maji safi na salama katika kijiji cha Kizuka na kuwataka wananchi kutunza mradi huo ili uendelee kuwa suluhisho la changamoto iliyokuwepo kwa muda mrefu ya huduma ya maji.
Amewaomba wa Jimbo la Peramiho,kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao Jenista Mhagama na kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha Waziri Aweso,amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mwajuma Waziri,kutoa Sh.milioni 300 ili kukamilisha mradi wa maji katika kijiji cha Lipokela na Lipaya.
Naye Katibu Mkuu wa wizara ya maji Mwajuma Waziri alisema,wizara ya maji itaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Peramiho wanapata huduma ya maji safi na salama.
“Mama yetu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,ametupa kazi ya kumtua mama ndoo kichwani,kwa hiyo tunawatoa hofu wananchi wa Kizuka na Jimbo la Peramiho kwa ujumla kuwa, miradi yote inakwenda kukamilika”alisema.
Mkazi wa kijiji cha Kizuka Agostino Mwanja,ameipongeza wizara ya maji kwa uamuzi wa kujenga mradi huo kwani kwa muda mrefu,wananchi wa kijiji hicho wana maisha magumu kutokana na kukosa maji ya uhakika.
Msimamizi wa ujenzi wa mradi wa maji Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea Hamis Yasin,akimuonyesha Waziri wa Maji Juma Aweso mchoro wa mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.730,430,012.76.
Waziri wa MajI Juma Aweso,akifungua koki kwenye moja ya vituo vya uchotea maji katika kijiji cha Kizuka wilayani Songea,baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),wa pili kulia meneja wa Ruwasa wilayani Songea Mathias Charles.
Waziri wa maji Juma Aweso,akimtua ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea Hilda Mhagama baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho.
Waziri wa Maji Juma Aweso,akiwa amjitwisha ndoo ya maji baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Kizuka wilayani Songea jana unaotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya Sh.milioni 730.