Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustwafa, akimkabidhi kipolo cha mchele mmoja wa wanachi wa Tumbatu aliepatwa na maafa ya upepo uliovuma katika kisiwa hicho siku za karibuni. (PICHA NA MPIGA PICHA).

NA FAUZIA MUSSA

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuzifariji familia 98 zilizoathiriwa na upepo mkali  uliovuma katika kijiji cha Tumbatu siku za karibuni.

Kufuatia tukio hilo   lililotokea mwishoni mwa mwezi wa Agosti, Taasisi ya Sister Island imekabidhi kilo 1350 za mchele kwa wananchi hao.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi chakula hicho, huko Kichanagani  katika Ofisi ya Wilaya ndogo Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Idrisa Kitwana Mustwafa, Alisema Serikali kwa ujumla imeguswa na tukio hilo, hivyo itaendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha hali za wanakijiji hao zinarudi kama zilivyokuwa awali.

Aidha aliwataka wananchi hao kuwa wastahmilivu wakati serekali ikiendelea kuchukua hatua  za kuwafariji kutokana na maafa hayo.

Kaimu huyo ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi alisema Serikali inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi iko pamoja na wananchi wake ikiwemo wa kijiji cha Tumbatu kwa hali zote na hivyo ujio wa Mkuu huyo katika kisiwa hicho  ni utekelezaji wa  agizo la Rais wa Zanzibar kuja kuwafariji wananchi wake.

Sambamba  na hayo Mkuu huyo aliishukuru tasisi ya Sister Island kwa kushirikiana  na Serikali kuwafariji wananchi  wake kutokana na maafa hayo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa  Sister Island   Haji Moh’d Ali  alisema kama sehemu ya jamii tasisi hiyo imeamua kuzifariji familia hizo kutokana kuguswa na tukio hilo .

Alifahamisha kuwa Taasisi hiyo itaendelea kufanya kazi  kwa kushirikiana na Serikali katika  kutatua  changamoto mbalimbali za jamii, na kuwashukuru wananchi na viongozi wa Mkoa huo kwa kupokea msaada huo na kuahidi  kuendelea  kuwa karibu na wananchi wakati wote.

Baadhi ya waathirika waliopatiwa msada huo akiwemo  Kombo Mwadin Khamis na  Miza Juma Haji walisema  wanafarijika kuona wadau mbalimbali kwa kushirikiana  na Serikali  wapo karibu nao tangu yaliopotokea maafa hayo hadi kufikia sasa.

Itakumbukwa kuwa Agosti 22, 2024, upepo mkali ulivuma katika kisiwa cha Tumbatu na kuathiri mkaazi ya watu, nyumba za ibada na baadhi ya vipando katika mashamba ya wakulima wa kijiji hicho