Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI kilichojengwa mwaka 1959 katika eneo la Ndengu, Wilayani Mbinga kwenye Mkoa wa Ruvuma kimeelekezwa kufufuliwa ili kianze shughuli za uzalishaji wa mbegu za ngano, tafiti za mbegu za mpunga na muhogo, pamoja na upimaji wa afya ya udongo.
Ameelekeza hayo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo aliposimama kukikagua wakati wa ziara yake katika Wilaya za Nyasa na Mbinga tarehe 20 Septemba 2024.
Waziri Bashe ameongeza zaidi kuwa Mkurugenzi wa TARI Uyole, Dkt. Tippe ahakikishe Kituo hicho kitakufufuliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo (ASA) ili kuzalisha mbegu kwa wingi kusaidia wakulima wa Wilaya hizo mbili ambao wanafanya kilimo cha kahawa, mpunga, muhogo, michikichi, mahindi na mazao mengine.
Naye Dkt. Tippe ameomba Watumishi wa tatu wa Kituo hicho wapatiwe pikipiki kusaidia usafiri; ambapo ombi hilo Mhe. Waziri Bashe aliridhia na kuielekeza Wizara ya Kilimo iwapatie pikipiki tatu.
Aidha, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) nayo imeelekezwa kusaidia upatikanaji wa mbolea za ruzuku ili wakulima wa eneo hilo waweze kunufaika kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mbegu za ruzuku zisambazwe kwa wakulima na kwa wakati.
[9/21, 12:36 AM] Tagie Daisy HGCU Kilimo: SERIKALI KULETA MAPINDUZI TASNIA YA KAHAWA
Serikali imewahakikishia wakulima na wamiliki wa viwanda vya kukoboa Kahawa nchini kuwa itatengeneza utararibu wa kuuza kahawa ili kuwa na mfumo wa uwazi wenye bei itakayomnufaisha mkulima kwa kuchagua bei anayoitaka.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) alipofanya ziara ya ukaguzi katika Kiwanda cha Kupokea na Kukoboa Kahawa aina ya “Arabica” (Mbinga Coffee Curing Company) kilichopo Mbinga, mkoani Ruvuma tarehe 20 Septemba 2024.
“Lazima tuongeze tija kwa wazalishaji wa kahawa. Hivyo, niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kutoa miche ya ruzuku ya kahawa ambayo inazalishwa na TACRI, tutaanzisha mfumo wa ruzuku za pembejeo, tutachimba visima kusaidia wakulima na kujenga ghala la kuhifadhi kahawa zao,” amesema Waziri Bashe.
Kuhusu wafanyabiashara wanyonyaji kwa wakulima (kangomba), Serikali itachukua hatua dhidi ya unyonyaji huo kwa wakulima. Waziri Bashe amesema kuwa ushirika imara siyo unaonyonya wakulima; na hivyo wakulima kupitia vyama vya ushirika na waliopo katika vikundi mbalimbali washiriki katika mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) linalosimamia mnada wa kijiditali ili kuwaongezea uhakika wa masoko, uhuru wa kuamua bei, uhakika wa malipo yao pamoja na kuchochea ushindani.
Aidha, Waziri Bashe amehamasisha wazalishaji wa Kahawa nchini kama vile aina ya Mbinga Café kuwa na kampeni bunifu za kunadi upekee / utofauti wa kubidhaisha Kahawa zao ili kuvutia biashara. Ametolea mifano kama vile hadithi au simulizi kuhusu Kahawa ya kampuni fulani, au viungo / ladha / virutubisho vilivyomo kwenye Kahawa husika.
Mbinga Coffee Curing Company inamilikiwa na Vyama vya Ushirika 28 vinavyolima Kahawa nchini kwa asilimia 56.54, huku Serikali ikimiliki asilimia 43.46 ambapo kiwanda chake kilianza ukoboaji wa Kahawa mwaka 1989. Kiwanda kina uwezo wa kukoboa tani 10 kwa saa moja, na uwezo wa kukoboa tani 30,000 kwa mwaka.