Wamiliki wa vyombo vya moto nchini wametakiwa kuhakikisha Madereva wa vyombo hivyo wanafuata sheria za usalama barabarani na kuacha mara moja tabia ya kuendesha magari ya abiria na mizigo bila kukagua magari wanayoyaendesha ili kubaini mapungufu yaliyonayo.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 17, 2024 na Mkuu wa Operesheni Kikosi cha Usalama barabarani nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nassor Sisiwaya alipokuwa kituo cha ukaguzi wa Magari Chimbuya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe kwenye operesheni maalumu za ukaguzi zinazoendelea nchini kote.
Vilevile, ACP Sisiwaya amewataka madereva kukagua magari yao kabla ya kuanza safari pia aliwataka wamiliki wote wa vyombo hivyo vya moto kuhakikisha magari yao yanakaguliwa na kupata stika ya NENDA KWA USALAMA.
Naye, Kaimu Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, Mkaguzi wa Polisi Fidelia Kasongwa amesema kuwa, Jeshi la Polisi limebaini na kuyakamata magari ya mizigo na abiria 07 ambayo mifumo yake ya breki haipo sawa na kupelekea madhara kwa abiria na chombo kutokana na mazingira ya Mkoa wa Songwe kuwa na milima, miteremko na kona nyingi ambapo gari lisipokuwa na breki linaweza kuleta madhara kwa dereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Aidha, Mkaguzi wa Magari wa Polisi Mkoa wa Songwe Koplo Samwel Mtatiro amewakumbusha wamiliki wote wa magari kuwakumbusha mara kwa mara madereva wao kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani pindi wawapo safarini na kufichua utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya madereva wengine ambao unahatarisha usalama kwa watumiaji wengine wa barabara ambapo amewataka watumiaji wote wa vyombo vya moto kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa salama wakati wote.
Kwa upande wake dereva mmoja wapo aliyekamatwa kwa kosa la mfumo wa breki amesema kuwa tatizo hilo linatokana na ubovu wa barabara za nchi jirani ambazo zinapelekea matairi kuisha na kupata tatizo la kufeli breki na kuwaomba matajiri wa magari hayo kuweza kuyatengeneza ili kuwa salama kwenye safari zao wakati wote kwa lengo la kuepusha madhara kwenye jamii na miundombinu ya barabara.