MKUU wa wilaya Kaskazini ‘A’, Othman Ali Maulid, akipokea zawadi ya ndizi kutoka kwa Pandu Mahmoud Pandu mwanachama wa mtandano wa wakulima wadogo wadogo (MVIWATA) katika Mkutano wa mwaka kanda ya Zanzibar uliyofanyika baraza la mji wilaya ya kaskazin B Kinduni. (PICHA NA MPIGA PICHA)
NA FAUZIA MUSSA
WAKULIMA wadogo wadogo wametakiwa kutumia fursa za mahoteli yaliopo nchini kuuza bidhaa zao ili kujiinua kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya kaskazini ‘A’, Othman Ali Maulid, wakati akizungumza na wakulima hao katika mkutano wa mwaka wa mtandao wa vikundi vya wakulima wadogo wadogo (MVIWATA) kanda ya Zanzibar uliofanyika Kinduni katika ukumbi wa mikutano wa baraza la mji wilaya ya kaskazini ‘B’ Unguja alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Alieleza kuwa serikali zote mbili zinaendelea kuimarisha miundoni ya kilimo ili kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao yenye tija, yanayoendana na mahitaji ya hoteli.
Aidha aliviisitiza vikundi hivyo kushirikiana kwa pamoja katika kuelezea changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wadogo wadogo ili kuleta mageuzi ya kilimo.
Mwenyekiti wa vikundi vya wakulima wadogo kanda ya Zanzibar, Hadia Ali Makame alisema mtandao huo ni chombo cha kitaifa kinachowaunganisha wakulima wadogo wadogo kupitia vikundi ili kuwa na sauti ya pamoja kutetea maslahi yao katika nyanza zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
“umoja huu umefanikiwa kuwaunganisha wakulima wadogowadogo unguja na pemba na kupata fursa mbalimbali ikiwemo kushiriki katika skukuu ya wakulima nane, kutoa mapendekezo yao katika baraza la wawakilishi kufuatia mwaliko wa baraza hilo na sasa tumepata nmafasi ya kuwapelekea vijana wetu wawili kushiriki mafunzo ya kilimo mkoani Morogoro” Alisema
Mjumbe wa bodi MVIWATA Taifa Namri Najim Jecha alisema taasisi hiyo itaendelea kuchukua juhudi za kuwaunganisha wakulima hao na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili Kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
“bado kuna changamoto ya mwamko mdogo wa ushiriki wa wakulima wadogo wadogo hasa kutoka kisiwa cha pemba, kama MVIWATA tunaahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ili Kila Mkulima anufaike katika mtandao huu”
Wakulima walioshiriki katika mkutano huo akiwemo Tatu Juma Rubishi kutoka wilaya ya Magharibi A,Omar Maabad Ali kutoka wilya ya kaskazini B Unguja na Husein Ismail Ndevu kutoka wilaya ya kati walisema wanakosa mitaji ya kutisha, elimu ya kilimo, masoko kushuka pamoja na ardhi kuharibika kutokana na baadhi ya mbolea wanaozitumia, hali ambayo walilitaja kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Hivyo waliomba serikali na wadau mbali mbali kuendelea kuwaunga mkono wakulima wadogo wadogo ili kuzalisha bidhaa zenye viwango zitakazo kidhi mahitaji ya jamii na wawekezaji.
Mkutano huo uliambatana na uchaguzi wa viongozi wa kanda ya Zanzibar ambapo wanachama 76 walipiga kura na Hadia Ali Makame kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa MVIWATA kwa kura 75 Kati ya 76 zilizopigwa.