Afisa Muuguzi wa kituo cha afya Litumbandyosi Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Songela Songela kulia,akimuonyesha Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt Seleman Jumbe wa pili kushoto na katibu wa afya wa Halmashauri Dickson Simangwe kitanda cha kujifungulia kwa akina mama wajawazito wanaofika kupata huduma hiyo,wa pili kulia Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt Jackline Zugra.
Baadhi ya majengo ya kutolea huduma za afya katika kituo cha afya Litumbandyosi kata ya Litumbandyosi Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma ambayo ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh.milioni 500 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Muonekano wa jengo la wodi ya wazazi katika kituo cha Afya Litumbandyosi Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,Halmashauri ya wilaya imetumia zaidi ya Sh.milioni 500 kujenga kituo cha kisasa cha afya kama mkakati wake wa kuboresha huduma za afya na kuwaondolea adha wakazi wa kata hiyo kusafiri umbali mrefu kwenda maeneo mengine kufuata huduma hizo.
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
WAKAZI wa kata ya Litumbandyosi Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wameondokana na adha ya kutembea umbali wa kilometa 85 kufuata huduma za afya Mbinga mjini baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha afya Litumbandyosi kilichogharimu Sh.milioni 500.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Dkt Seleman Jumbe alisema,kituo hicho kimejengwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya wilaya ni kinahudumia zaidi ya wakazi 15,000 wa kata ya Litumbandyosi na maeneo ya jirani.
Dkt Jumbe alitaja majengo yaliyojengwa katika kituo hicho ni jengo la wagonjwa wa nje(OPD)maabara,wodi ya wazazi kwa ajili ya kulaza na kujifungua,jengo la kufulia nguo,kichomea taka na kufunga jenereta.
“Sisi kama Halmashauri ya wilaya Mbinga tunaishukuru Serikali,wananchi wa kata ya Litumbandyosi na vijiji vya jirani wamepata msaada mkubwa kwa kuwepo kwa kituo hiki kwani kimesaidia wananchi kutoangaika tena kwa kwenda maeneo ya mbali kufuata huduma za matibabu”alisema Dkt Jumbe.
Kwa mujibu wa Dkt Jumbe,tangu kituo kilipofunguliwa mwezi mei mwaka huu kimesaidia sana kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto kwani hapo awali baadhi ya mama hao walipoteza maisha njiani kabla ya kufika kwenye maeneo ya kutolea huduma za afya.
Amewaomba wananchi wa kata ya Litumbandyosi, kuhakikisha wanatunza majengo hayo na watumishi kutunza vifaa vilivyopo ili vidumu kwa muda mrefu na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika kupata matibabu.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Jackline Zugra alisema,tangu kituo hicho kilipoanza kutoa huduma mwezi Mei mwaka huu vifo vya mama wajawazito vimepungua kwani wanaofika kujifungua kwa mwezi ni kati 18 hadi 20 na hakuna mama mjamzito au mtoto aliyepoteza maisha.
Alisema,mbali na mama wajawazito wanatoa huduma za kawaida ambazo awali zilitolewa kwenye zahanati ndogo na wale waliohitaji huduma za upasuaji walisafirishwa kwenda Mbinga na Hospitali ya Peramiho na Hospitali ya rufaa ya mkoa Songea(Homso).
Mkazi wa kijiji cha Mabuni kata ya Litombandyosi Regina Mapunda alisema, kituo hicho cha afya ni ukombozi mkubwa kwa kuwa kimewasaidia watu wengi hasa wanawake wajawazito wa kata hiyo kujifungua salama na kupungua kwa vifo vya mama na mtoto kwa kujifungulia njiani kabla ya kufika kwenye vituo vya kutolea huduma.
Aidha alisema,kituo hicho kimepunguza gharama kubwa walizokuwa wanatumia kutoka Mabuni kwenda Hospitali ya wilaya Mbinga mjini umbali wa kilometa 85 na Hospitali ya Misheni Peramiho wilayani Songea iliyopo umbali wa kilometa 55.
“Serikali ya awamu ya sita imetufanyia jambo kubwa sisi wananchi wa kata ya Litumbandyosi, kwani awali tulitegemea kupata huduma za afya kwenye zahanati ndogo ya kijiji iliyojengwa miaka zaidi ya 50 iliyopita”alisema Mapunda.
Alisema,katika zahanati changamoto kubwa ilikuwa kukosekana kwa huduma muhimu zikiwemo za mama na mtoto na upasuaji,hivyo walipohitaji kwenda Hospitali kubwa walitumia kati ya Sh.90,000 hadi 100,000 kukodi gari kwenda maeneo Mbinga mjini au Peramiho kufuata huduma.
Mapunda,ameiomba Serikali kuongeza huduma muhimu kama za upasuaji,gari la wagonjwa na watumishi zitakazowezesha wananchi kupata huduma bora zaidi za afya zinazolingana na ubora wa majengo yaliyojengwa.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Nehema Komba,ameshukuru kujengewa kituo cha afya lakini alisema, gari la wagonjwa ni muhimu sana kuwepo katika kituo hicho ili liweze kutumika pale wagonjwa watapopewa rufaa kwenda Hospitali kubwa kwa ajili ya uchunguzi kwa kuwa kijiji chao kipo mbali na maeneo ya mjini.
Thobias Komba,ameipongeza Serikali kwa jitihada za kujenga kituo cha afya,lakini ameshauri kuongezwa watoa huduma wengi na vifaa tiba ili kuepusha usumbufu unaoweza kutokea kwa kwenda maeneo mengine kufuata baadhi ya huduma ambazo hazipo katika kituo hicho.