WAZIRI wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro,akifungua Mdahalo wa Kitaifa wa Maadili uliofanyika katika ukumbi wa Chandamali Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ikiwa ni kuelekea Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika kuanzia Septemba 20 – 23, 2024 katika uwanja wa Majimaji Songea.
Baadhi ya washiriki wa Mdahalo wa Kitaifa uliofanyika katika ukumbi wa Chandamali Manispaa ya Songea
Na Mwandishi Wetu
Songea
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amewataka Watanzania kutumia utandawazi kuongeza maarifa katika kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa, badala ya kuacha utandawazi kuharibu utamaduni wa Taifa letu.
Dkt Ndumbaro amesema hayo jana,wakati akifungua Mdahalo wa Kitaifa wa Maadili uliofanyika katika ukumbi wa Chandamali Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ikiwa ni kuelekea Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika kuanzia Septemba 20 – 23, 2024 katika uwanja wa Majimaji Songea.
Amesema Tanzania ina mila na desturi zake ambazo ni tofauti na mataifa mengine na kusisitiza kuwa wizara ina muongozo wa maadili katika shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo ndani na nje ya Tanzania.
“Taifa lisilokuwa na Utamaduni wake ni mfu” haya ni maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Rais wetu wa sasa, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kutoa msisitizo kwa jamii kufuata mila na desturi za jamii ambapo kupitia maelekezo yake kwa wizara kuwa na Tamasha la Utamaduni kila mwaka kwa mikoa tofauti.
Ameongeza kuwa, utamaduni ndio msingi wa maadili pia ni mfumo wa uongozi, chakula, mavazi, elimu, sherehe, utamaduni usioshikika na unaoshikika.
Waziri Ndumbaro,ametoa wito kwa wana Ruvuma kujitokeza kwa wingi katika Tamasha hilo ambapo mgeni rasmi siku ya kilele Septemba 23, 2024, atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni katika wizara hiyo Boniface Kadili amesema, Mdahalo huo ni sehemu ya utekekezaji wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambapo amesema sera hiyo inaeleza wajibu wa jamii katika kuenzi, kulinda na kukuza mila na desturi.
Naye Afisa Utamaduni Mwandamizi wa Kitengo cha Urithi na Maadili ya Taifa wa Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Tito Lulandala ameyataja maazimio ya mdahalo huo ni wazazi kuwajibika vema katika malezi ya Watoto wao na jamii iweke mkazo zaidi katika malezi na makuzi yenye maadili.
Maazimio mengine ni kuchukua hatua kuhusu mmomonyoko wa maadili kwa wanasiasa katika ngazi zote wahamasishe uwajibikaji wa familia na jamii yote kwa ujumla katika kurithisha maadili mema kwa Watoto na vijana, jamii kulinda maadili na kuhakikisha malezi na makuzi bora ili wasiige tamaduni za kigeni.
Alisema, wazazi na walezi kuelimisha watoto kuhusu madhara ya matumizi yasiyokuwa sahihi ya Sayansi na teknolojia ikiwemo mitandao ya jamii,viongozi wa dini kuhakikisha wanaifundisha jamii maadili mema,wazazi kuwa mfano wa kushiriki kwenye matukio ya kijamii ikiwemo mikutano ya wazazi shuleni na wazazi na walezi kuwa karibu na Watoto wao ili kujua changamoto zinazowakabili na kutengeneza mazingira rafiki kwa Watoto ili wataja changamoto zao.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoani Ruvuma Dkt.Primius Nkwera amesema maadili mema na upendo vikitawala katika familia vinaweza kupunguza mmomonyoko wa maadili huku akisisitiza sheria ichukue mkondo wake kwa watu wote wanaovunja sheria na kusababisha maadili mabovu.
Naye Shekhe wa Mkoa wa Ruvuma Ramadhani Mwakilima ameutaja utamaduni na maadili kuwa vinajengwa na dini ambapo amesisitiza mizizi mikuu ya maadili mema ni wazazi na walezi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mathias Tilia amesema, ili kuwa na maadili mema mafundisho ya msingi ya malezi kwa Watoto yaimarishwe.
Kwa ujumla jamii nzima wakiwemo wazazi,walezi,viongozi wa dini,walimu,wanasiasa na wadau wote wanatakiwa kusimamia maadili mema ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.
Mdahalo huo umeongozwa na mada mbalimbali zikiwemo za athari za mmomonyoko wa maadili kwa maendeleo ya jamii, nafasi ya viongozi wa kisiasa na kijamii katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili pamoja na umuhimu wa maadili kwa maendeleo ya jamii