NA FAUZIA MUSSA
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Ofisi ya Pemba wametakiwa kusimamia maadili ya utumishi na kujiepusha na vishawishi vitakavyopelekea kuathiri utendaji wao wa kazi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed wakati akizungumza na Wafanyakazi hao huko Gombani, Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Kamishna Said alisema watendaji hao wanawajibu wa kusimama katika njia za uadilifu na haki ili kutimiza majukumu yao ipasavyo ikiwemo Ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Kaimu Kamishna Mkuu aliwataka watendaji hao kuzisoma na kuzielewa Sheria za kodi wanazozisimamia ili kuitendea haki Serikali na Walipakodi Kwa ujumla.
“bila ya kuzisoma na kuzingatia sheria hizi, mtashindwa kukusanya mapato Jambo ambalo litapelekea upotevu wa mapato ya Serikali kwa kutokana na kushindwa kusimamia Sheria za kodi.” alisema
Pamoja na kusimamia Sheria na mapato ya Serikali, wafanyakazi hao walisisitizwa kusimamia haki za Walipakodi kwa kuhakikisha wanatenda haki bila ya kumuonea Mlipakodi wala kuteteresha mapato ya Serikali.
Mkurugenzi Ofisi ya ZRA Pemba, Jamal Hassan Jamal alisema ofisi hiyo ilikadiriwa kukusanya Shilingi 47.971 bilioni Kwa mwaka 2024-2025 ambapo kwa miezi miwili ya mwanzo ya mwaka huo imeweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni nane sawa na wastani wa asilimia 103.84 ya makadirio Hali inayoonesha ufanisi katika utendaji.
Aidha alisema Ofisi ya ZRA Pemba itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia lengo la kukusanya bilioni 42 kupitia Vyanzo mmbalimbali ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Ushuru wa Utalii na Ushuru wa Mafuta.
Nao watendaji wa Ofisi ya ZRA Pemba waliupongeza Uongozi wa ZRA kwa miongozo wanayoitoa na kuaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato Stahiki yatakayowezesha kutoa huduma bora kwa jamii.