Na WMJJWM-SAME
Wanawake nchini wamehamasishwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi sambamba na kupiga kura ili kupata Viongozi wenye sifa watakaoshija nafasi mbalimbali za uongozi.
Hayo yamesemwa Wilayani Same mkoani Kilimanjaro na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis wakati akifungua Kongamano la Wanawake Wilayani humo.
Mhe. Mwanaidi amesema kongamano hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali ya kukutana na wadau kuzungumza na kupeana uzoefu wa mambo mbalimbali na namna bora ya kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali nchini.
“Kwa kutambua umuhimu wa kundi hili, Wanawake watafahamishwa juu ya uwepo wa fursa za biashara, ufikiaji wa masoko na namna ya kupata na kukuza mitaji. Nitoe rai kwa wanawake na wananchi wote, kutumia fursa hizi vizuri kwa lengo la kuongeza wigo wa wanawake waliojiajiri ili nanyi muweze kuajiri watu wengine.” amesema Naibu Waziri Mwanaidi
Amesisitiza Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya 2023 inayobainisha dira ya Serikali kuhusu masuala ya wanawake ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa Programu ya Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa lenye lengo la kuongeza chachu ya kufikia Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi amewahamasisha Wanawake Wilayani humo kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za matumizi ya mishafi safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali ili kusaidia kutunza mazingira, kuokoa muda, kuimarisha afya na Uchumi.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi amewahamasisha Wanawake wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Wizara ambapo jumla ya Shillingi bilioni 10.5 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo wanawake.
“Niwaombe wanawake wote mliopo hapa mjitokeze kutambuliwa na kusajiliwa katika mfumo mpatiwe vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo ndogo ili muweze kupata fursa ya mkopo inayotolewa katika sekta ya umma na binafsi hususani benki ya NMB ambayo tumeingia nayo ubia wa kutoa mikopo hiyo.” amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi