BAADHI ya bidhaa zilizokamatwa zikiwa zimepitwa na muda wa matumizi kufuatia ukaguzi uliofanywa na ZFDA
NA FAUZIA MUSSA
WAKALA wa Chakula na Dawa (ZFDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamefanikiwa kukamata bidhaa za vyakula na vipodozi zilizokwisha muda wa matumizi katika maduka mbalimbali ya mkoa wa mjini magharibi.
Bidhaa hizo ni pamoja na mafuta ya kula tani 1 ,bia ,maharage na mahindi ya makopo ,sweet cone ,maziwa ya maji ya kopo , pamoja na tambi vilivyopatikana katika ghala la kampuni ya Cross Border Trading Company Limited lililopo Tomondo, wilaya ya Magharibi ‘B’.
Bidhaa nyengine zilizokamatwa katika zoezi hilo ni sabuni na vipodozi vilivyopatikana katika maduka mbalimbali maeneo ya darajani, wilaya ya Mjini.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo huko Ofisi za ZFDA Mombasa, Mkurugenzi Idara ya udhibiti usalama wa chakula na ufanisi Dk. Khamis Ali Omar alisema kufuatia ukaguzi huo wamebaini uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wanaoendesha shughuli hizo bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Alieleza kuwa bidhaa nyingi zilizokamtwa katika ukaguzi huo zimebainika kumaliza muda wa matumizi na nyengine kupigwa marufuku kutokana na kuwa na viamabata sumu mbalimbali ndani yake na kuwa sio salama kwa matumizi ya Binaadamu.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa Mfanyabiashara wa ghala hilo amebainika kufanya udanganyifu katika bidhaa zilizomaliza muda wa matumizi kwa kubadilisha tarehe ya muda katika bidhaa hizo.
“Baadhi ya bidhaa hapa zinaelekeza ukitaka maelezo ya muda wa matumizi yapo chini ya bidhaa hii, ukiangalia utakuta michubuko inayoashiria maelezo hayo yamefutwa na badala yake unakutana na kikaratasi chembamba cha maelezo ya muda wa matumizi karibu na ufiniko wa bakuli la bidhaa hii” alisema
Dk. khamis alieleza kuwa Taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuangalia uhalali wa wafanyabiashara na usalama wa bidhaa, na kila wanapofanya ukaguzi hukutana na matukio kama hayo ambapo bidhaa za chakula zinaonekana kuongoza kwa kuuzwa kinyume na utaratibu ikiwa ni pamoja na kupitwa na muda wa matumizi .
Hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara kuacha tabia ya kuuza bidhaa zilizokwisha muda wake kwani jambo hilo hupelekea athari kwa watumiaji.