Na John Bukuku, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamoud Thabit Kombo, ameweka wazi mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni nchini China, ambayo inabeba umuhimu mkubwa kwa Tanzania na Afrika.
Akielezea mafanikio hayo akiwa nchini China Kombo amesimulia kuhusu Mkutano wa tisa wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) uliofanyika nchini humo hivi Kombi amesema kuwa wengi hawaelewi umuhimu wa China kufanya mkutano na bara zima la Afrika. Lakini, Rais wa China aliweka wazi sababu kuu – Afrika, ikiwa na nchi 54, inawakilisha nguvu kubwa yenye idadi ya watu bilioni 1.4, sawa na idadi ya watu wa China.
“Rais wa China alifafanua kuwa, japokuwa China ni nchi moja, tunashiriki kitu kimoja kikubwa – idadi ya watu. Hilo ndilo linatufanya tuungane kwa karibu. Afrika ina watu bilioni 1.4, na China pia ina watu bilioni 1.4. Tunaposhirikiana, inakuwa ni ‘watu kwa watu’. Tanzania, ikiwa na watu milioni 62, ni sehemu muhimu ya huu ushirikiano wa kipekee,” alieleza Kombo kwa msisitizo.
Akiendelea kusimulia, Kombo amegusia jinsi Rais wa China alivyoonyesha pongezi kubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Alimueleza kuwa mmoja wa viongozi bora barani Afrika, akisema kwamba miradi inayosimamiwa na Tanzania chini ya ushirikiano wa China imefanikiwa kwa kiwango cha juu bila kukumbana na changamoto zozote.
“Rais wa China alimsifu Rais Samia kwa kuwa mfano bora wa uongozi barani Afrika. Alibainisha kuwa miradi yote iliyotekelezwa kwa ushirikiano na China imekamilika kwa mafanikio makubwa, bila vikwazo vyovyote. Hii si kazi ya siku moja; tumesherehekea miaka 60 ya urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na China, na urafiki huo umetupeleka mbele zaidi ya nchi nyingi za Afrika,” amesema Kombo.
Mafanikio ya ziara hiyo hayakuishia hapo tu. Kombo alielezea kuwa Rais Samia na Rais wa China walitia saini makubaliano mapya ambapo China imeahidi kutoa dola bilioni 4.5 za Kimarekani ili kuendeleza ushirikiano kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania, ambayo tayari imekuwa ikitia fora katika utekelezaji wake.
“Rais wa China alitamka wazi kuwa Tanzania imetoa mfano wa kipekee katika usimamizi wa miradi, na sasa ni mfano unaoigwa na nchi nyingine za Afrika. Tumefanikiwa kufungua mlango mkubwa wa maendeleo na ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili, na matarajio ni kuona mafanikio haya yanachochea ukuaji zaidi wa kiuchumi na kijamii,” alihitimisha Kombo.
Ni wazi kuwa ziara hiyo inaifanya Tanzania izidi kuimarika katika ushirikiano wake wa kimataifa, na matunda yake yatakuwa na athari kubwa kwa wananchi wake na kwa sekta mbalimbali za maendeleo. Ni hadithi ya mafanikio ambayo kila Mtanzania anapaswa kuifahamu na kujivunia.