Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Equality for Gowth(EFG) ,Jane Magigita akizungumza na wanawake katika wiki ya AZAKI.
Mwenyekiti wa soko la Kiwalani ,Neema Charles akizungumza na wanawake katika wiki hiyo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.ASASI mbalimbali za kiraia zimeombwa kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa wanawake ili waweze kutambua haki zao na kujiamini pamoja na kuwa na udhubutu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi .
Aidha wamesema kuwa ,elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu kwani wengi wao hawajiamini na wamekuwa wakiogopa kuwania nafasi mbalimbali kutokana na changamoto zilizopo.
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Equality for Gowth(EFG) ,Jane Magigita wakati akitoa mada katika wiki ya AZAKI inayoendelea mkoani Arusha.
Magigita amesema kuwa,pamoja na elimu mbalimbali ambayo imekuwa ikitolewa na mashirika mbalimbali kwa wanawake bado uhitaji wa elimu hiyo ni mkubwa na nguvu zaidi inahitajika kuongezwa ili wanawake zaidi waweze kufikiwa kwani kuna wengine ambao bado hawajafikiwa kabisa.
Amesema kuwa, EFG ni shirika linaloendeleza usawa wa ukuaji kiuchumi,usawa wa kijinsia ,na kuwajengea uwezo wa kisheria na kibiashara wanawake walio katika sekta hiyo rasmi nchin Tanzania.
Ameongeza kuwa ,dira ya shirika hilo ni kuona hakuna vikwazo vyovyote vya kijinsia kwa wanawake walio katika sekta isiyorasmi na wanawake wakiwa mbali na aina zote za unyonyaji.
Akiendelea kutoa mada amesema kuwa,malengo makuu ni kusaidia jamii ili kuona wanawake na wanaume wana haki na nafasi sawa ya kumiliki Mali na shughuli za kiuchumi ,utawala na kuinua maendeleo ya sheria za uchumi na kijamii.
Ameongeza kuwa, wamekuwa wakihamasisha na kusaidia wanawake walio katika nyanja ya kiuchumi kujenga umoja na uwakilishi wao kwa lengo la kuwapa uwezo wa kuwa wajasiriamali na kutambua haki zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko la Kiwalani ,Neema Charles amesema kuwa,wao kama wanawake wameweza kujiamini na kupata ujasiri mkubwa baada ya kupata elimu kutoka shirika hilo ambapo hapo awali walikuwa na hofu ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kutokana na kutojiamini na kuona wanaume pekee ndo wanafaa.
“Kwa mfano mimi nilikuwa naogopa kabisa kugombea nafasi yoyote kwa kujionea kuwa sitaweza wanaume tu ndo wanaweza ,lakini baada ya kupata hii elimu kutoka shirika hili nimeweza kuwa na ujasiri mkubwa na kuweza kugombea nafasi ya uongozi na nimepata na nawawakilisha vyema wanawake wenzangu kwa kutetea haki zao katika maeneo yao ya kazi.”amesema Neema .
Amesema kuwa, katika wiki hii ya AZAKI wameweza kujifunza maswala mbalimbali ambayo hawakuwa na uelewa nayo huku akiwataka wanawake wajiamini kuwa wanaweza na kuwa na udhubutu wa hali ya juu katika kugombea nafasi mbalimbali.
Naye Mwakilishi kutoka shirika la EFG ,Prisca Mwaiko amesema kuwa, ni vizuri wadau mbalimbali wakashirikiana na asasi hizo katika kutoa elimu zaidi kwa wanawake ili waweze kufahamu haki zao kwani kuna wengine ambao hawajafikiwa na elimu.hiyo .