KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Gerson Msigwa,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati akizungumza nao leo Septemba 10,2024 jijini Dodoma kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Gerson Msigwa,akizungumza leo Septemba 10,2024 jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Kitaifa la Utamaduni linalotajia kuanza Septemba 20, na kumalizika Septemba 23,mwaka huu Mkoani Ruvuma ili kuimarisha Utamaduni uliopo nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Gerson Msigwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10,2024 jijini Dodoma kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Bw.Msigwa amesema kuwa Kaulimbiu ya tamasha hilo itakuwa ni ‘Utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza, Kazi iendelee’ Tamasha linaratibiwa na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo waratibu wa Tamasha la Majimaji Serebuka, kutoka mkoani, Ruvuma Songea.
“Tamasha hilo litafunguliwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro,Septemba 20,mwaka huu na kilele chake itakuwa Septemba 23,mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”amesema Bw.Msigwa
Amesema kuwa Tamasha hilo limekuwa na faida nyingi kwa jamii ambazo ni pamoja na; kuenzi utamaduni wetu, kuimarisha utangamano wa kitaifa, kuitangaza nchi yetu, kutangaza vivutio vya kiutalii na kiutamaduni, fursa za kiuchumi, na kijamii, kutanua wigo na mitandao ya kibiashara kwa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani bidhaa za utamaduni, sanaa, na ubunifu.
“Madhumuni ya tamasha hili ni pamoja na; kuenzi na kulinda utamaduni wetu, kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukuzaji wa sekta za ubunifu na utamaduni, kutoa jukwaa la kuonyesha utamaduni kama msukumo madhubuti wa utangamano wa kitaifa kwa kuwaleta/kuwaunganisha pamoja wadau na viongozi wa sekta, kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni wetu, kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa, kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa na kutangaza fursa na rasilimali za kipekee ilizonazo nchi yetu.”amesema
Aidha ameongeza kuwa Tamasha la mwaka huu litakuwa na vionjo mahsusi kama vile mirindimo ya kiasili, kuanzia mavazi, maonesho, visasili na visakale.
“Tamasha litakuwa na mdahalo wa kitaifa utakaozungumzia mapambano dhidi ya viashiria vya mmomonyoko wa maadili na nini mchango wa jamii katika kupunguza na hatimaye kuondoa viashirika hivyo:”amesema
Hata hivyo ameeleza kuwa Tamasha litakuwa na onesho maalumu la matumizi ya kanga ikiwa ni vazi la utamaduni wa Mtanzania na zaidi ya vikundi 25 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar; vikundi hivyo ni vya sanaa ya asili, ubunifu, utamaduni na mziki wa kizazi kipya.
Pia Tamasha litakuwa na mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania Bara na visiwani pamoja na kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
” Kutokana na umuhimu na mvuto wa tamasha hili, naomba na kuwahakikishia kampuni zote, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kujitokeza kudhamini tamasha hilo.”
Bw.Msigwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahususi ya kufungamanisha utamaduni na utalii, utamaduni na biashara, utamaduni na uchumi kwa ujumla.
“Kwa ujumla, tamasha hili ni fursa muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisayansi, kisiasa na kiutamaduni. Aidha, ni njia mahususi ya kukuza viwanda vya ubunifu sanaa na utamaduni nchini. Tamasha linaandaliwa katika namna ya kuzitangaza tunu zetu, vivutio vyetu vya kiutamaduni, tunaomba sana ushirikiano wa watanzania wote.”ameeleza Bw.Msigwa