Na Mwamvua Mwinyi
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Michael Manumbu amefungua rasmi mashindano ya Polisi Jamii (Polisi Jamii Cup) kwa Mkoa wa Pwani ambapo yamefanyika katika viwanja vya Wilaya ya Kipolisi Chalinze yakiwa na kauli mbiu *”Kuzuia na Kupambana na Uhalifu ni Jukumu letu katika Jamii”.
Akifungua mashindano hayo Septemba 09,2024 Kamishna Manumbu alieleza kuwa lengo kuu la mashindano hayo ni kutoa elimu kwa wananchi na kupata taarifa za uhalifu na wahalifu hivyo kuzuia vitendo hivyo kwa kiwango kikubwa.
ACP Manumbu alieleza kuwa elimu ya Haki Jinai ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi wataelimishwa ili wafahamu haki zao ikiwemo haki ya dhamana ambayo hutolewa bure katika vituo vyote vya Polisi huku akiwataka wananchi wanapopata changamoto vituoni wawasiliane na viongozi wa Polisi ili wasaidiwe.
Sambamba na hayo, ACP Manumbu alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Afande Camillius Wambura -IGP kwa kuona na kukubali mashindano hayo yafanyike ili elimu ifike kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali na alimpongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Pius Lutumo kwa kuridhia mashindano haya yafungiliwe rasmi katika Wilaya ya Kipolisi Chalinze.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bwilingu, Chalinze, Bw Nasar Hemed Kalama alitoa Pongezi kwa Jeshi la Polisi kwani uhalifu katika maeneo ya Chalinze umepungua kwa kiasi kikubwa kwani elimu inayotolewa ikishirikisha Jeshi la Polisi na viongozi wa vijiji imesaidia sana kupunguza matukio ya uhalifu.
Mashindano hayo yalizinduliwa kwa mchezo wa mpira wa miguu kati ya Chalinze FC na CHAUWA FC ambapo timu ya Chalinze FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 4 kwa 1.