Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mkoani Manyara Mhe Edward Ole Lekaita amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ametaja mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo kampeni ya kumtua ndoo mama kichani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo la Kiteto umeongezeka.
Mbunge Ole Lekaita ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndirigishi mara baada ya kuzindua shule mpya ya sekondari Ndirigishi.
Amesema kuwa kwa mafanikio ya miradi mbalimbali Rais Samia anaenda kuandika historia kubwa katika jimbo la Kiteto na nchi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa katika uongozi wa Rais Samia Shilingi Bilioni 1 imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule na mabweni katika shule hiyo ya sekondari Ndirigishi, Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo vya Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Kiteto, Bilioni 1 kwa ajili wa ujenzi wa soko la mazao Engusero na Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Hali kadhalika, Mbunge Ole Lekaita amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote katika Wilaya ya Kiteto, pia amesema kuwa zaidi ya madarasa 200 yamejengwa katika kipindi cha uongozi wake huku shule shikizi 18 zikiwa zimejengwa na kusajiliwa huku Shule mpya 2 za msingi zikiwa zimejengwa katika Kata ya Matui na Dongo.